Posted by Esta Malibiche on Nov 15,2016 in NEWS
Na
Jacquiline Mrisho.
Mkuu
wa Wilaya ya Chato iliyopo mkoani Geita, Shaban Ntarambe amekiri kuwa
ushirikiano wa shirika la Plan International katika kudhibiti ajira hatarishi
za watoto umefanikiwa kumaliza tatizo hilo katika Kijiji cha Msasa.
Hayo
yamesemwa leo mkoani Geita na Mkuu huyo alipokuwa akiongea na mwandishi wa
habari hii juu ya mchango wa Mradi wa Uondoaji Ajira Hatarishi na Vitendo vya
Ukatili kwa Watoto unaofadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD) na
kuratibiwa na shirika la plan International jinsi ulivyowasaidia wananchi wa
Kijiji hicho.
Ntarambe
amesema kuwa ushirikiano wa Shirika hilo, jamii pamoja na uongozi wa migodi iliyopo
kwenye Kijiji hicho umesaidia katika kuhakikisha elimu ya ajira, afya na
usalama kwa watoto inatolewa, hivyo kupitia elimu hizo wananchi wamepata uelewa
juu ya athari za ajira za watoto na kujumuika katika uzuiaji wa ajira hizo.
“Tumefanikiwa
kwa asilimia zote kuzuia ajira za watoto katika eneo hilo ambalo lina
mkusanyiko mkubwa wa wachimbaji wa madini, kimsingi ni kwa sababu ya
ushirikiano unaotolewa na shirika la Plan International kwani wanatoa
rasilimali nyingi zinazowezesha kufanikisha kuondoa tatizo hilo”, alisema
Ntarambe.
Akiongea
kuhusu suala la athari wanazopata watoto wadogo wanaobebwa na mama zao
wanaofanya kazi migodini amesema kuwa wanasaidiana na shirika hilo katika
kuwapatia elimu pamoja na mitaji ili
waachane na kazi za migodi na badala yake watafute kazi mbadala za kujitafutia
vipato ili kuwakinga watoto wadogo wasiathiriwe na kazi zinazofanyika katika
maeneo hayo.
Kwa
upande wake Mratibu wa Mawasiliano wa Shirika hilo, Raymond Kanyambo
amemshukuru Mkuu wa Wilaya hiyo kwa kutambua umuhimu wa shirika hilo na kuahidi
kuendelea kushirikiana nae katika kutatua matatizo yanayowakabili wananchi wa
wilaya hiyo haswa katika masuala ya unyanyasaji wa watoto na ukatili unaofanywa kwa wanawake.
“Shirika
letu linahusika na kutetea haki za watoto, hivyo tuliona ni vyema kupeleka
nguvu zetu katika maeneo yenye migodi kwa kuwa ni maeneo yanayoongoza katika
utoaji wa ajira za watoto walio na umri chini ya miaka 18, mradi huu
ulitekelezwa katika wilaya za Nyan’ghwale na Geita lakini baada ya kuona mafanikio
tumeamua kuiongeza wilaya ya Chato ili kukomesha kabisa tatizo hili”, alisema
Kanyambo.
Mradi
huu wa miaka mitatu una lengo la kuondoa ajira hatarishi na vitendo vya ukatili
kwa watoto wanaoishi karibu na maeneo ya migodi, umeanzishwa Novemba 2015 na
utagaharimu jumla ya Euro 1,500,000 hadi kuisha kwake.
0 maoni:
Chapisha Maoni