Jumatano, 30 Novemba 2016

Prof. Ole Gabriel: Sekta ya kilimo mkombozi ajira kwa vijana

Posted by Esta Malibiche on Nov 30,2016 in NEWS
04
Sekta ya kilimo nchini imekuwa mkombozi kwa ajira ya vijana kwa asilimia 81.18 ilikinganishwa na sekta nyingine ambapo idadi ya vijana kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Mkazi ya 2012 wapo vijana milioni 16.2 huku idadi ya vijana wa kike wakiwa milioni 8.3 na wa kiume milioni 7.9 
Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Prof. Elisante Ole Gabriel amesema hayo leo jijini Mbeya wakati wa mkutano wa wadau wa maendeleo kwa lengo la kuwajengea uwezo vijana wenye umri wa miaka 18 hadi 30 ulioitishwa na taasisi isiyo ya kiserikali ya TechnoServe chini ya Mradi wa Uimarishaji wa Maendeleo ya Vijana Vijijini kupitia Biashara (STRYDE).
Akielezea mgawanyo wa ajira kwa vijana nchini, Prof. Ole Gabriel amesema kuwa sekta ya Umma nchini inaajiri vijana 188,000, sekta binafsi vijana 1,027,000 wakati vijana wanaojiajiri ni 1,100,000.
Prof. Ole Gabriel amesema kuwa taasisi ya TechnoServe kupitia mradi wake wa STRYDE imekuja na mbinu ambayo imewapa kipaumbele vijana wengi na kuwapa elimu ya kujitambua ili wabadili utamaduni wao wa kufikiri waweze kuchangamkia fursa za kiuchumi zilizopo katika maeneo yao.
01
Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Prof. Elisante Ole Gabriel akiongea na wadau wa maendeleo (hawapo pichani) jijini Mbeya wakati wa mkutano wa  kuwajengea uwezo vijana wenye umri wa miaka 18 hadi 30 ulioitishwa na taasisi isiyo ya kiserikali ya TechnoServe chini ya Mradi wa Uimarishaji wa Maendeleo ya Vijana Vijijini kupitia Biashara (STRYDE).
Katika kuinua vijana kichumi, Prof. Ole Gabriel amesema kuwa mwanadamu ana sehemu kuu mbili ambazo ni sehemu inayoonekana (mwili) na sehemu isiyoonekana inayoshughulika na fikra ambayo inamsaidia mwanadamu katika kuboresha maisha yake pamoja na jamii yake.
“Shughulikeni na sehemu isiyoonekana ya vinjna ndiyo muhimu, mkifanya hayo mtawakomboa vijana na taifa” alisema Prof. Ole Gabriel.
Kufuatia sehemu hizo kuu za mwanadamu, taasisi ya TechnoServe imekuwa msatari wa mbele katika kuhakikisha inamjengea uwezo vijana kujua na kutumia fursa walizo nazo kwa kubadili fikra zao katika kufanyakazi.
Prof. Ole Gabriel amewapongeza TechnoServe kupitia mradi wake wa STRYDE kwa kuwainua vijana kifikra na kubadilisha mfumo wao wa maisha ambalo hilo ni jambo la kuigwa na kujivunia.
02
Katibu Tawala wa Mkoa wa Mbeya Bi. Mariam Mtunguja akimkaribisha mgeni rasmi Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Prof. Elisante Ole Gabriel wakati wa mkutano ulioitishwa na taasisi isiyo ya kiserikali ya TechnoServe chini ya Mradi wa Uimarishaji wa Maendeleo ya Vijana Vijijini kupitia Biashara (STRYDE).
Vilevile ametumia fursa hiyo ya kukutana na vijana kwa kumpongeza kijana Clementina Jairo mwenye umri wa miaka 23 kutoka Wilaya ya Rungwe mkoani Mbeya kwa kuwa balozi mzuri wa mradi huo kwa kufanya kazi za ujariamali kwa ujasiri mkubwa ambapo alianza kilimo cha kibiashara kwa mtaji wa sh.2000 na sasa anamiliki mtaji wa akiba ya sh.500,000 katika Benki ya NMB.
Akitoa taarifa ya taasisi yake kwa Mgeni Rasmi Mkurugenzi Mkazi wa TechnoServe nchini Bi. Alexandra Mandelbaum amesema kuwa taasisi hiyo itaendelea kushirikiana na Serikali katika kutatua tatizo la ajira kwa vijana kwa kuwajengea uwezo kifikra ili waweze kuendesha maisha yao ambapo kwa sasa wanatoa mafunzo kwa vijana katika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini.
Bi. Alexandra amesema kuwa TechnoServe inatarajia kuwafikia vijana 15,430 ifikapo 2019 ambapo mradi wa kuwajengea uwezo vijana kiuchumi unatekeleza kwa miaka mitano kuanzia mwaka 2014.
03
Mkurugenzi Mkazi wa TechnoServe nchini Bi. Alexandra Mandelbaum akitoa taarifa ya taasisi yake na kuahidi wataendelea kushirikiana na Serikali katika kutatua tatizo la ajira kwa vijana kwa kuwajengea uwezo kifikra ili waweze kuendesha maisha yao jijini Mbeya.
Awali akimkaribisha Mgeni Rasmi, Katibu Tawala wa Mkoa wa Mbeya Bi. Mariam Mtunguja amkakikishia Mkurugenzi Mkazi wa TechnoServe nchini kuwa Serikali ya mkoa wa Mbeya itaendelea kuwapa ushirikiano ili kuhakikisha mkoa huo unapambana na adui umasikini kwa kubadilisha fikra za vijana katika maendeleo yao na taifa kwa ujumla.
Aidha, Bi Mariam ameongeza kuwa wataweka mazingira wezeshi ya kijinsia na kijamii kwa vijana ili waweze kuzitumia fursa zilizopo katika kujiongezea kipato.
Kwa upande wake kijana Clementina Jairo ambaye ni mnufaika wa mafunzo ya STRYDE amesema kuwa ndoto yake ni kuwa mjasiriamali mkubwa anatarajia kufanya biashara ya pembejeo za kilimo na kuwa mkulima wa kilimo cha kisasa.
Mradi wa Uimarishaji wa Maendeleo ya Vijana Vijijini kupitia Biashara (STRYDE) unatekelezwa katika nchi nne za Afrika Mashariki ambazo ni Tanzania, Kenya, Uganda na Rwanda chini ya ufadhili wa MasterCard Foundation.
04
Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Prof. Elisante Ole Gabriel akimpongeza kumpongeza kijana Clementina Jairo mwenye umri wa miaka 23 kutoka Wilaya ya Rungwe mkoani Mbeya kwa kunufaika kwa Mradi wa Uimarishaji wa Maendeleo ya Vijana Vijijini kupitia Biashara (STRYDE) ambapo ameanza kilimo cha kibiashara kwa mtaji wa sh.2000 na sasa anamiliki mtaji wa akiba ya sh.500,000 katika Benki ya NMB.
05
Mkurugenzi Mkazi wa TechnoServe nchini Bi. Alexandra Mandelbaum (kushoto) akimpongeza Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Prof. Elisante Ole Gabriel (kulia) mara baada ya kutoa hutuba wakati wa mkutano jijini Mbeya.
06
Kijana Clementina Jairo kutoka Wilaya ya Rungwe mkoani Mbeya akitoa ushuhuda namna alivyonufaika na Mradi wa Uimarishaji wa Maendeleo ya Vijana Vijijini kupitia Biashara (STRYDE) ambapo ameanza kilimo cha kibiashara kwa mtaji wa sh.2000 na sasa anamiliki mtaji wa akiba ya sh.500,000 katika Benki ya NMB.
07
Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Prof. Elisante Ole Gabriel akiwa katika picha ya pamoja mara baada mkutano na wadau wa Mradi wa Uimarishaji wa Maendeleo ya Vijana Vijijini kupitia Biashara (STRYDE) jijini Mbeya.(Picha na Eleuteri Mangi,- WHUSM, Mbeya)

0 maoni:

Chapisha Maoni