Jumamosi, 12 Novemba 2016

AMINA MASENZA;ZINGATIENI ULAJI UNAOFAA ILI KUJIKINGA NA KISUKARI

 Posted by Esta Malibiche on nov 12,2016 in NEWS




Na Esta Malibiche
Iringa
Wananchi  Mkoani Iringa wametakiwa kuzingatia ulaji unaofaa wa vyakula ili kujikinga na Magonjwa mbalimbali ukiwemo ugonjwa  wa Kisukari.

Akizungumza katika mahojiano maalum ofisi kwake kuhusu maandalizi ya kilele cha Siku ya Kisukari Duniani Mkuu wa Mkoa wa Iringa Amina Masenza alisema kuwa Mkoa wa Iringa kama maeneo mengine Duniani unaadhimisha siku hii, kwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa kupima wananchi wake ili waweze kufahamu hali zao na pia kutoa elimu ya umuhimu wa kuzuia na kujikinga na madhara yatokanayo na ugonjwa wa kisukari.

Masenza alisema Ulaji unaofaa ni kula chakula mchanganyiko cha kukutosha kukua na kuwa na uzito wa kawaida na chenye virutubisho vyote vinavyohitajika mwilini. Kwa mfano vyakula vya wanga vinasaidia kuupa mwili nguvu na joto, protini husaidia kujenga mwili na kutengeneza vichocheo mbalimbali, vitamin na madini hulinda mwili dhidi ya magonjwa.


‘’’’Wananchi wetu lazima kujiepusha na kula vyakula bila kuzingatia aina na kiasi kulingana na mahitaji ya mwili. Ulaji huu huweza kusababisha kupungua au kuzidi kwa virutubishi mwilini. Ulaji usiofaa ni pamoja na kula vyakula vyenye mafuta mengi hasa yale yatokanayo na wanyama, kula vyakula vyenye chumvi nyingi, sukari nyingi, kula chakula kupita kiasi, kukoboa nafaka na kutokula mbogamboga na matunda kiasi cha kutosha’’’’Alisema Masenza


AlisemaMambo yanayoongeza uwezekano wa kupata magonjwa yasiyo ya kuambukiza ni pamoja na ulaji usiofaa hasa matumizi ya chumvi kwa wingi, mafuta na sukari, uzito uliozidi, unene uliokithiri, kutofanya mazoezi, uvutaji wa sigara na bidhaa zitokanazo na tumbaku, unywaji pombe kupita kiasi na msongo wa mawazo.

‘’’’Ili kuzuia ugonjwa wa kisukari na maradhi mengine yasiyo ya kuambukiza ni muhimu kufuata kanuni za afya ambazo ni ulaji bora, na mtindo bora wa maisha ambao ukifuatwa vyema huweza kwa kiasi kikubwa kuzuia mtu kupata kisukari au kwa mtu ambaye tayari ana ugonjwa wa kisukari hupunguza uwezekano wa kupata madhara makubwa ya kiafya’’’




Aidha aliongeza kuwa Siku ya Kisukari Duniani ilianzishwa mwaka 1991 na Mashirika mawili ya kimataifa yaani World Health Organization (WHO) na International Diabetes Federation (IDF) baada ya kuona ugonjwa wa Kisukari unaongezeka sana Duniani na Siku hiyo huadhimishwa Duniani kote kila mwaka ifikao tarehe 14 Novemba.

‘’’’Ugonjwa wa Kisukari ni hali ambayo hutokea wakati sukari katika damu inapokuwa nyingi kupita kiwango cha kawaida kwa muda mrefu. Sukari hutumiwa na mwili ili kupata nishati lishe. Ili mwili uweze kutumia sukari inayotokana na vyakula, unahitaji kichocheo cha insulin. Insulin husaidia sukari kuingia kwenye chembechembe hai ili kutengeneza nishati lishe. Ugonjwa wa kisukari unasababishwa na kichocheo hiki kupungua au kutofanya kazi kama inavyotakiwa, hivyo kiwango cha kisukari kinabaki kikubwa kwenye damu kwa sababu sukari haikuwezeshwa kuingia kwenye chembechembe hai za mwili’’’’’


Alisema kuwa Mara nyingi, watu wengi hawajitambui kuwa wana ugonjwa huu. Wengine wanakuwa na dalili lakini hawachukui hatua mapema. Dalili za kisukari ni rahisi kuzitambua.

‘’’’Dalili hizo ni kiu isiyoisha, kukojoa mara kwa mara, kupungua uzito, kusikia njaa kila wakati na mwili kukosa nguvu. Mwananchi yeyote akiwa na dalili hizi aende hospitali au katika kituo cha Afya ukapime sukari’’’’Alisema Masenza

Alisema katika bara la Afrika kulikuwa na wagonjwa wa kisukari 19.8 millioni mwaka 2013 na wataongezeka mpaka million 41.4 ifikapo mwaka 2035, ambapo nusu ya wagonjwa hawa walikuwa hawajaanza matibabu. Asilimia 80 ya wagonjwa wote wa kisukari ulimwenguni wanaishi katika nchi zinazoendelea, ikiwemo Tanzania.

‘’’’Mwaka 2012 Hypertension Prevalence ilikuwa karibu 26% na Kisukari ilikuwa karibu 20%. Mwaka 2010 vifo vilivyotokana na Magonjwa yasiyoambukizwa Tanzania vilikuwa 27%. ‘’’’Alisema Masenza



Alisema Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa inaendelea na  Kliniki ya kupima ugonjwa wa Kisukari na Shinikizo la Damu kwa wananchi wa Manispaa ya Iringa na maeneo yanayozunguka Manispaa hiyo.
‘’’’Kliniki hiyo ilizinduliwa rasmi tarehe 10/11/2016,na itaendelea kwa siku TANO mfululizo hadi tarehe 14/11/2016 siku mbayo ni kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Kisukari Duniani’’’Alisema Masenza.

0 maoni:

Chapisha Maoni