Posted by Esta Malibiche on Nov 12,2016 in NEWS
Na: Lilian Lundo – MAELEZO – MARA
Mradi wa bustani za mbogamboga
katika shule ya Msingi Mazoezi Bunda iliyoko kata ya Nyasura, wilaya ya
Bunda Mkoani Mara unaingizia shule hiyo kiasi cha shilingi 50,000 hadi
100,000 kwa kila mwezi.
Mwalimu Mkuu wa shule hiyo Vicent
Ndunguru aliyasema hayo Wilayani Bunda wakati wa mahojiano na timu ya
wilaya inayosimamia mpango wa kuinua ubora wa elimu wilayani humo.
“Shule imeweza kujitunzia akiba
ya fedha ambapo kabla ya mradi wa bustani za mbogamboga shule haikuwa na
akiba yoyote lakini baada ya kuanzisha mradi huo, shule haikosi kuwa na
akiba ya kiasi cha shilingi 50,000 mpaka 100,000 kwa mwezi,” alifafanua
Mwalimu Ndunguru.
Mwalimu Ndunguru aliendelea kwa
kusema kuwa, kutokana na mradi huo shule imeweza kujinunulia vifaa vya
kufundishia kama vile chaki.
Pia fedha nyingine imekuwa
ikitumika kutoa motisha kwa wanafunzi wanaofanya vizuri katika masomo
pamoja na kutoa huduma ya kwanza kwa mwanafunzi au mwalimu anayepata
tatizo na kuhitaji matibabu ya haraka.
Aidha mradi huo umewajengea uwezo
wa kujitegemea wanafunzi wa shule hiyo na kupelekea idadi kubwa ya
wanafunzi wa darasa la sita kuanzisha bustani za mbogamboga majumbani
kwao na kutumika kama chanzo cha mapato cha familia.
Mwalimu Ndunguru amewashauri
walimu, kamati za shule na wazazi nchini kuwa wabunifu na kuanzisha
miradi mbalimbali kama vyanzo vya mapato ambavyo vitasaidia kuendesha
shughuli za elimu katika shule zao.
0 maoni:
Chapisha Maoni