Posted by Esta Malibiche on Nov 8,2016 in NEWS
Mkuu
wa kikosi cha Usalama Barabarani mkoa wa Arusha (SSP) Nuru Kacharia
akitoa takwimu juu ya hali ya usalama barabarani kwa wananchi wa Arusha
wakati wa uzinduzi ya wiki ya nenda kwa usalama barabarani iliyofanyika
jana katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha. (Picha na Rashid
Nchimbi wa Jeshi la polisi Arusha)
Kamanda
wa polisi Mkoa wa Arusha Naibu Kamishna (DCP) Charles kumbo akitoa
shukrani kwa wadau wa kampuni mbalimbali wakiwemo na waandishi wa habari
katika kufanikisha sherehe za wiki ya nenda kwa usalama barabarani.(
Picha na Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha)
Mkuu
wa wilaya ya Arusha Mh. Gabriel Daqarro (aliyekaa katikati mwenye suti)
ambaye alimwakilisha Mkuu wa mkoa kwenye uzinduzi ya wiki ya Nenda kwa
Usalama Barabarani mkoani Arusha akiwa katika picha ya pamoja na wadau
mbalimbali. (Picha na Rashid Nchimbi wa jeshi la Polisi Arusha)
Askari wa Kikosi cha Usalama Barabarani Koplo Athilio Choga akimuelezea
mgeni rasmi mkuu wa wilaya ya Arusha Mh. Gabriel Daqarro (Mwenye suti)
namna ya mpangalio wa mji unavyoweza kupanua barabara ili kuepukana na
ajali.(Picha na Rashid Nchimbi wa jeshi la Polisi Arusha)
Askari
wa Brass Bendi ya Polisi toka Chuo cha Polisi Moshi wakiwa wanatoa
heshima jukwaani wakati wakipita mbele ya mgeni rasmi Mh. Gabriel
Daqarro mkuu wa wilaya ya Arusha wakati wa uzinduzi ya wiki ya Nenda kwa
usalama Barabarani mkoani hapa (Picha na Rashid Nchimbi wa Jeshi la
Polisi Arusha)
………………………………………………………………..
Na Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha
Katika
kipindi cha toka Januari mpaka Oktoba mwaka 2016 ajali za vifo
zimepungua kwa asilimia ishirini na nne ukilinganisha na kipindi kama
hicho mwaka 2015, ambapo kulikuwa na jumla ya ajali za vifo 74 tofauti
na mwaka huu kumekuwa na ajali 56 ambapo ni sawa na upungufu ya ajali 18
ambazo ni 24% .
Akitoa
takwimu hizo katika sherehe za uzinduzi ya wiki ya nenda kwa Usalama
Barabarani zilizofanyika katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Mkuu wa
kikosi cha Usalama Barabarani mkoani hapa Mrakibu Mwandamizi wa Polisi
(SSP) Nuru Kacharia alisema kwamba katika ajali hizo 74 kwa mwaka 2015
jumla ya watu 97 walipoteza maisha na mwaka huu 2016 kwa kipindi kama
hicho ajali hizo ni 56 ambazo zilisababisha vifo vya watu 68.
Kacharia
aliendelea kubainisha kwamba, mbali na upungufu wa ajali za vifo lakini
kikosi hicho cha Usalama Barabarani kwa kushirikiana na wadau
mbalimbali wameweza pia kupunguza ajali za majeruhi kwa 5% ambapo mwaka
2015 kuanzia Januari hadi Oktoba ajali zilizosababisha majeruhi zilikuwa
763 tofauti na ajali zilizosababisha majeruhi 725 kwa kipindi kama
hicho kwa mwaka huu wa 2016.
“Asilimia
75 ya ajalli za barabarani zinasababishwa na wanadamu kwa kutotii
sheria za barabarani, madereva kuendesha vyombo vya usafiri wakiwa
walevi, kuendesha kwa mwendokasi, watembea kwa miguu na waenda
mikokoteni kutofuata sheria”. Alifafanua Mkuu huyo wa Usalama
Barabarani.
Alisema
mbali na makosa ya kibinadamu lakini pia, ubovu wa vyombo vya usafiri
kama vile uchakavu wa magurudumu na kadhalika husababisha ajali kwa
asilimia kumi na tano pamoja namiundo mbinu ya barabarainachangia kwa
asilimia kumi.
Alisema
kwamba kwa mwaka huu wa 2016 Kikosi cha Usalama Barabarani kwa
kushirikiana na wadau mbalimbali wa vyuo vya udereva wameweza kutoa
elimu kwa jumla ya wadereva 73,830 wa vyombo vya usafiri, huku vituo
2,149 vya pikipiki wanachama wake walipata elimu sahihi ya matumizi ya
barabarani, na kuongeza kwamba jumla ya vipindi 624 vya redio sawa na
dakika 18,720 zilitumika katika kuwaelimisha watumiaji wa barabara kwa mwaka huu wa 2016.
Akizindua
rasmi wiki ya nenda kwa Usalama Barabarani mkoani hapa, kwa niaba ya
Mkuu wa Mkoa wa Arusha mara baada ya ukaguzi wa vibanda mbalimbali
vilivyomo ndani ya uwanja huo, Mkuu wa wilaya ya Arusha Mh. Gabriel
Daqarro alisema kwamba ajali za barabarani zimeendelea kugharimu maisha
ya watu wengi hivyo kuathiri ustawi wa jamii pamoja na uchumi kwa
ujumla.
Alisema
kila mmoja wetu anapaswa kuchukua hatua ili kupunguza ajali na kuiagiza
kamati na taasisi husika kuweka mikakati madhubuti kama vile
kupendekeza marekebisho ya sheri za usalama barabarani, wakala wa
barabara waweke alama za barabarani ili zitoe uelewa sahihi kwa
watumiaji wa barabara na kuliomba Jeshi la Polisi washirikiane na wadau
wengine liweze kutoa mafunzo ya mara kwa mara hasa kwa waendesha
pikipiki ili ajali hizo ziweze kupungua.
Kwa
upande wake Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha Naibu Kamishna (DCP)
Charles Mkumbo ambaye pia ni mlezi wa Kamati ya Usalama Barabarani
alisema kwamba, kamati hiyo itatekeleza yote yaliyoagizwa na Mkuu wa
Mkoa na kuwashukuru wadau wote pamoja na vyombo mbalimbali vya habari
kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi kikosi cha Usalama barabarani na
kuahidi kuongeza jitihada za kila aina ili kuweza kupunguza ajali .
Katika
sherehe hizo za uzinduzi zilizokuwa na kauli mbiu “Hatutaki ajali
tunataka kuishi salama” Jeshi la Polisi liliwatunuku vyeti wadau
mbalimbali pamoja na Mtangazaji wa kituo cha Televisheni cha Star
TV mkoani hapa Ramadhani Mvungi na Radio Triple “A” kwa kutoa mchango
mkubwa katika uelimishaji wa jamii juu ya Usalama Barabarani mkoani
hapa.
0 maoni:
Chapisha Maoni