Posted by Esta Malibiche on Nv 4,2016 in NEWS
Na: Genofeva Matemu – WHUSM
Mwenye macho haambiwi tazama na
anayeshindwa kushukuru kwa jambo dogo hata akifanyiwa jambo kubwa kwake
yeye ataliona dogo kwa sababu amedhamiria kutokuwa na roho ya kuridhika.
Novemba Tano mwaka 2016 ni mwaka
mmoja tangu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe
Magufuli alipoapishwa kuwa Rais na Amri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi
na Usalama wa Nchi hii ambapo ameweza kufanya mambo makubwa kiasi
kwamba ukipingana na hali halisi basi utaonekana kuwa mtu usiyekuwa na
shukrani kwa kila jambo.
Hatua hii inaonyesha kuwa katika
kipindi cha mwaka mmoja wa uongozi wake toka aingie madarakani amekua
mstari wa mbele kuhakikisha mafanikio makubwa yanapatikana katika sekta
ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kupitia viongozi wanaosimamia
sekta hizo pamoja na serikali kwa ujumla.
Baada ya kuapishwa kwake Rais wa
Serikali ya Awamu ya Tano aliona umuhimu wa sekta ya Sanaa hivyo kuamua
kuiundia Idara ili sekta hiyo iweze kusimamia kwa karibu kazi za Sanaa
na kuwafanya wasanii kupata haki halali kupitia kazi za zao.
Katika hali ambayo haikutarajiwa
na watu wengi, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Nape
Moses Nnauye hakusita kufanya ziara ya kushtukiza kwa wafanyabiashara wa
kazi za Sanaa maeneo ya Soko la Kariakoo akiwa na lengo la kuwafichua
wafanyabiashara wote wa kazi za Filamu na Muziki ambazo hazina stika za
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) zinazoashiria uhaliali wa kazi hizo.
Mhe. Nnauye anasema kuwa, hatua
hii ni ya mwanzo kwa kuwaonyesha kuwa agizo la Rais wa Serikali ya Awamu
ya Tano, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli la kulipa kodi kwa bidhaa zote
zilizopo sokoni pamoja na kununua bidhaa halisi kwa kudai risiti
linasimamiwa na kutekelezwa ipasavyo.
Ili kuua soko haramu la kazi za
filamu na muziki wito kwa watanzania ulitolewa na Mhe. Nnauye kuwa tuwe
na tabia ya uzalendo kwa kununua bidhaa za filamu zenye stampu ya TRA
ili kusaidia katika kukusanya kodi na kuinua uchumi wa nchi lakini pia
kuinua kipato cha wasanii.
Sanjari na hilo Serikali ya Awamu
ya Tano kupitia Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
imedhamiria pia kurasimisha kazi ya sanaa kuwa shughuli rasmi ya
kiuchumi katika kipindi cha miaka mitano ya uongo wa Rais Dkt. John
Pombe Magufuli.
Ili kuwezesha hilo Mhe. Nnauye
amewaomba wadau mbalimbali kujitokeza kudhamini mashindano ya kuibua
vipaji vya sanaa huku akiahidi kuendeleza sekta ya sanaa nchini ili
kuwezesha vijana wengi kutambua vipaji vyao na kuweza kujiajiri na
kuajiri wengine kupitia kazi za sanaa.
Wakale uneni msina kwao mtumwa.
Lugha aushi na adhimu ya Kiswahili imeongeza mawanda mapya ndani ya
mwaka mmoja wa Serikali ya Awamu ya Tano ambapo Bunge la Afrika
Mashariki (EALA) limekubali hoja ya kuifanya lugha ya Kiswahili kuwa
lugha rasmi katika shughuli za bunge la Afrika Mashariki hatua hiyo
dhahiri inayounga mkono pendekezo la mwenyekiti wa wakuu wa Jumuiya hiyo
Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli.
Akizungumzia hoja hiyo Mbunge wa
EALA Mhe. Shayrose Banji amekiri Bunge la Afrika Mashariki limekubali
kuifanya lugha ya Kiswahili kuwa lugha rasmi lakini haswa kuienzi na
kuithamini lugha hii ambayo ndiyo pekee inayozungumzwa katika nchi zote
za Jumuiya na hata nchi zilizo nje ya Jumuiya.
Aidha, Mbunge wa EALA kutoka
Tanzania Mhe. Adam Kimbisa amesema kuwa hapa Tanzania Kiswahili
kinatumika kwa asilimia zaidi ya 95, Kenya zaidi ya asilimia 80, Uganda
zaidi ya asilimia 50, Rwanda zaidi ya asilimia 50 na Burundi zaidi ya
asilimia 60 hivyo ni wakati muafaka kwa Bunge hilo kuridhia lugha hii
kuwa rasmi ndani ya Bunge.
Katika kuunga mkono jitihada za
Serikali ya Awamu ya Tano katika kukuza lugha ya Kiswahili, Kanisa
Katoliki nchini liliandaa Kamusi ya Ukristo iliyoandikwa na Padre Jordan
Nyenyembe na kuzinduliwa rasmi na Serikali mwezi Agosti mwaka 2016.
Uzinduzi wa Kamusi hiyo utasaidia siyo tu uelewa wa imani na kukua kwa
lugha ya Kiswahili, bali pia kuchochea upendo na amani nchini kwa
kutumia lugha ya Kiswahili iliyopo ndani ya kamusi hiyo.
Dhahiri Serikali ya Awamu ya Tano
imeonyesha umuhimu wa lugha ya Kiswahili kwa kukutana na manguli,
majagina na mangwiji, wakongwe na wapenzi wa lugha ya Kiswahili kujadili
changamoto zinazoikabili tasnia ya lugha ya Kiswahili nchini na
kupendekeza jinsi ya kuzitatua changamoto hizo katika kukubali na kuunga
mkono juhudi za Serikali katika kuishadidisha lugha adhimu ya
Kiswahili. Chambilecho cha Hayati Shaaban Robert alisema maajabu makuu
mawili sintayasahau “Ni Mwalimu Nyerere na Lugha ya Kiswahili”
Aidha Naibu Waziri wa Habari,
Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Anastazia James Wambura alisema kuwa
Serikali ya Awamu ya Tano imezingatia umuhimu mkubwa wa kuwa na Sera ya
Lugha ambayo ni mwongozo thabiti unaosimamia masuala yote yanayohusu
Lugha nchini ambapo kwa sasa Wizara inaendelea na mchakato wa uandaaji
wa Rasimu ya Sera ya Taifa ya Lugha iliyofikia hatua ya ukusanyaji wa
maoni ya awali ya wadau wa Lugha kwani tangu tulipopata uhuru mwaka 1961
masuala yahusuyo lugha katika nchi yetu yamezingatiwa kama kipengele
muhimu katika Sera ya Utamaduni ya mwaka 1997.
Pamoja na hayo katika kipindi cha
mwaka mmoja sekta ya habari imepata manufaa kwa upande wa Shirika la
Utangazaji la Taifa (TBC) ambapo Mhe. Nnauye ameutaka uongozi wa Shirika
hilo kurejea mkataba wao na Kampuni ya Startimes wanayoshirikiana nao
baada ya kubainika kuwepo na upungufu hivyo kuufanyia marekebisho
mkataba huo ili kusaidia TBC kuboresha mapato tofauti na ilivyokuwa
awali.
Aidha waziri huyo mwenye dhamana
na masuala ya Habari alizungumza na uongozi wa juu wa Startimes na
kuwataka kutekeleza maazimio ya mkataba wa awali wa kukamilisha ujenzi
wa jengo la TBC pamoja na kuboresha studio ya shirika hilo kuifanya
kuwa studio ya kisasa zaidi.
Sambamba na hayo uongozi huo wa
Startimes umeridhia kuanza kufanya mafunzo ya kubadilishana uzoefu na
wafanyakazi wa TBC kwa lengo la kuwaongezea ufanisi katika kutekeleza
kazi zao kupitia mifumo ya teknolojia ya kisasa.
Katika kuleta maendeleo ya sekta
ya habari serikali imekamilisha ndoto ya wanatansia wa habari kwa
kuwaletea Muswada wa Sheria ya Huduma za Habari wa mwaka 2016 uliokuwa
ukisubiriwa kwa zaidi ya miaka ishirini, ambapo Muswada huo umelenga
kuirasimisha sekta hiyo na kuifanya iweze kuheshimiwa kama tansia
nyingine tofauti na ilivyo sasa.
Muswada huo umesheheni mambo mengi
mazuri yatakayoweza kuinyanyua sekta hiyo ikiwemo kuanzishwa kwa Baraza
Huru la Habari ambalo litakuwa likisimamia waandishi wote wa habari kwa
kuwasajili, pia muswada utasaidia kuundwa kwa bodi ya ithibati ambapo
bodi hiyo itakuwa ikitoa vitambulisho vya waandishi wa habari na
kuishauri serikali katika mambo ya elimu ya mafunzo ya wanahabari.
Serikali ya Awamu ya Tano katika
kipindi cha mwaka mmoja imeanzisha mfumo wa tiketi za elektroniki katika
uwanja wa Taifa ikiwa na lengo la kuongeza mapato lakini pia kukidhi
huduma ya haraka kwa wananchi wote watakaotumia Uwanja wa Taifa katika
matukio mbalimbali ya michezo.
Akizungumza wakati wa ukaguzi wa
mfumo huo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
Prof. Elisante Ole Gabriel alisema kuwa mfumo wa elektroniki katika
Uwanja wa Taifa ni wa kisasa na unawawezesha watu wote kuingia uwanjani
ndani ya dakika 180 hivyo kuokoa muda wakati wa kuingia uwanjani.
Prof.Gabriel amesema kuwa kila
mashine inatumia sekunde mbili kumruhusu mteja kuingia uwanjani tofauti
na awali ambapo ilimlazimu mteja kupanga foleni kwa kutumia tiketi za
kawaida wakati wa kuingia uwanjani lakini pia mfumo huo ni kichocheo
kikubwa katika kuongeza mapato ya Serikali.
Rais huyu wa Serikali ya Awamu ya
Tano katika kuonyesha umuhimu wa michezo nchini ameweza kufanya
mazungumzo mazuri na Mfalme Mohammed VI wa Morocco ambapo mazungumzo
hayo yakaleta neema ya kujengewa uwanja wa mpira wenye thamani ya Dola
za Marekani milioni 80 (zaidi ya shilingi Bilioni 160) katika Mji wa
Dodoma utakaokuwa mkubwa kuliko Uwanja wa Taifa uliopo Jijini Dar es
Salaam.
Heko Rais wetu, Mhe. Dkt. John
Pombe Joseph Magufuli, heko viongozi wa Wizara ya Habari, Utamaduni,
Sanaa na Michezo kwa kufanya mambo makubwa na mazuri katika kila sekta
ndani ya mwaka mmoja. Ni ukweli usiopingika kuwa Serikali ya awamu ya
tano ipo kwa ajili ya kuujenga uchumi wa nchi yetu. Mungu ibariki
Tanzania, Mungu Mbariki Rais wetu, Mungu wabariki viongozi wote wa
Serikali ya Awamu ya Tano.
0 maoni:
Chapisha Maoni