Wanufaika wa Mikopo ya Elimu ya
Juu ambao tayari wapo katika ajira wametakiwa kurejesha marejesho ya
mikopo waliyopewa kutokana na mfuko wa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu
(HESLB) kutegemea fedha hizo kuendelea kuwakopesha wanafunzi wengine.
Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa
ameyasema hayo leo Bungeni, Mjini Dodoma alipokuwa akiwasilisha hotuba
ya kuhitimisha mkutano wa tatu wa Bunge la kumi na moja.
“Uwezo wa Bodi ya mikopo ya Elimu
ya Juu kuwahudumia walengwa unajengwa na fedha zinazotengwa kila mwaka
katika mipango na Bajeti pamoja na marejesho ya mikopo iliyoiva kutoka
kwa wanufaika,” alisisitiza Mhe. Majaliwa.
Aliendelea kusema kuwa Serikali
inaendelea kufanya maboresho ya kimfumo na kisheria ili kuimarisha
urejeshwaji wa mikopo. Aidha amewaagiza waajiri wote Nchini kutekeleza
wajibu wao wa kuingiza makato ya marejesho wa mikopo ya wanufaika kwa
wakati na kwa viwango vinavyotakiwa baada ya kuwasiliana na Bodi ya
Mikopo.
Vile vile Mhe. Majaliwa amesema
kuwa Serikali inaendelea kuimarisha mfumo wa utoaji wa mikopo kwa
wanafunzi wa elimu ya juu sambamba na kushughulikia changamoto
mbalimbali zilizopo katika Bodi ya mikopo ili kuhakikisha utoaji wa
mikopo unafanyika kwa ufanisi.
Pia Serikali inategemea kubadilisha utaratibu wa kutoa mikopo ili kuwafikia
wanafunzi wote wenye uhitaji zaidi wakiwemo yatima na wenye uwezo mdogo
kiuchumi bila kujali aina gani ya program wanazozisomea.
0 maoni:
Chapisha Maoni