Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu imeandaa kongamano la siku mbili la uwekezaji litakalojadili mipango madhubuti ya kuhakikisha Watanzania wanashiriki kikamilifu katika ujenzi wa uchumi wa nchi yao.
Kongamano hilo linatarajia kufanyika katika ukumbi wa Benki Kuu Jijini Dar es Salaam kuanzia tarehe 21 -22 Julai mwaka huu.
Hayo yamesemwa leo Jijiji Dar es Salaam na Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera na Uratibu) Dkt.Hamis Mwinyimvua wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari kuhusu kongamano hilo.
Dkt.Mwinyimvua alisema Serikali imepitisha Sera ya ushiriki wa watanzania katika sekta ya Mafuta na Gesi asilia, hatua ambayo itasadia wananchi wazawa kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa uchumi wa nchi yao.
“Msukumo mkubwa wa serikali kwa sasa ni kuongeza ushiriki katika uwekezaji unaochochewa na ugunduzi mkubwa wa gesi asilia katika kina kirefu cha bahari ambao utaweza kuwanufasha Watanzania,” alisema Dkt. Mwinyimvua.
Aidha alisema kuwa kutokana ushiriki huo wa Watanzania kuwa suala mtambuka na agenda endelevu, Serikali iliiagiza Baraza la Taifa la Uwezeshaji kuanzisha Idara ya ushiriki wa watanzania katika uwekezaji ambayo imeanza kutekeleza majukumu yake mwezi Novemba mwaka 2015.
Kwa upande wake Katibu Mtendaji Baraza la Taifa la Uwezeshaji, Beng’i Issa alisema kuwa katika kongamano hilo linatarajia kushirikisha jumla ya wajumbe 350 wakiwemo wafanyabiashara wa ndani na nje ya nchi, Watendaji wa Serikali Kuu na halmashauri za Miji na Majiji.
Akizungumzia kuhusu manufaa ya kongamano hilo, Beng’i alisema Watanzania watanufaika zaidi kwa kuwa wataongeza ujuzi na uzoefu katika kushirikiana na wafanyabiashara wakubwa waliopo nje ya nchi wanaojihusisha na sekta za mafuta, gesi, kilimo, fedha, bima, ujenzi na manunuzi ya umma.