Waziri
wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. William Lukuvi amemteua
Jaji Jacob Mwambejele wa Mahakama Kuu-Kitengo cha Biashara kuchunguza
mgogoro wa Kijiji cha Mabwegere na vijiji jirani vya Mfuru, Mbigiri,
Mandengwa, Dumila, Matongolo na Maboiga vilivyopo Wilayani Kilosa, Mkoa
wa Morogoro ili kupata suluhisho la kudumu la mgogoro ambao umedumu kwa
miaka takribani 27.
Waziri Lukuvi amemteua Jaji huyo kwa mamlaka yake chini ya kifungu 18 (1) cha Sheria ya Ardhi sura 113.
Uteuzi huo umefanywa leo jijini Dar es Salaam ukiwa ni wa kwanza katika juhudi za utatuzi wa migogoro ya ardhi nchini.
“Huu
ni uteuzi wa kihistoria kwani migogoro ya ardhi hapa nchi huwa
inatatuliwa kiutawala lakini kutokana na ugumu wa mgogoro huu imebidi
nimteue jaji kufanya uchunguzi baada ya kijiji cha Mabwegere kukataa
taarifa ya msuluhishi, Bwana Steven Mashishanga,” alisema Lukuvi.
Kwa
mujibu wa Waziri Lukuvi, mgogoro huu ni wa muda mrefu tangu 1989 na
umesababisha hasara kwa Taifa ikiwemo vifo vya watu, kuua wanyama na
uharibifu wa mazao.
Lukuvi
amesema kutokana na mgogoro huo kuwa kati ya migogoro mikubwa hapa
nchini imebidi jaji ateuliwe ili kufanya uchunguzi ambao utafanikisha
kumalizika kwa tofauti hizo.
Jaji
Mwambejele ataongoza timu ya watu wanane (8) ambao watafanya kazi ya
uchunguzi huko Kilosa Morogoro kwa siku 60, alisema Lukuvi.
Uchunguzi
huo utaangalia mambo kadhaa ikiwemo kama uanzishwaji wa kijiji cha
Mabwegere ulianzishwa kisheria, kama ulikuwepo usahihi wa kisheria
katika upimaji wa eneo hilo na kama wanakijiji walishirikishwa, alisema
Lukuvi.
Lukuvi
ameyataja maeneo mengine ya uchunguzi huu kuwa ni kuangalia kama
upimaji ulizingatia mipaka, kuchunguza maeneo mengine yenye migogoro na
kuchunguza jambo jingine lolote ambalo litasaidia katika kuleta suluhu
ya mgogoro huo.
Aidha,
Lukuvi amewataka watu wa maeneo husika yenye mgogoro kutoa ushirikiano
kwa Jaji na timu yake wakati wa uchunguzi ili kuweza kuchangia katika
kupata suluhisho la kudumu.
Kwa
upande wake Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dkt. Steven Kebwe amemshukuru
Waziri Lukuvi kwa hatua aliyochukua kushughulikia mgogoro huo ambao
umechukua muda mrefu na kugharimu maisha ya watu na mali zao ikiwemo
mifugo na mazao.
“Nitashirikiana
na Jaji pamoja na timu yake ili kuhakikisha tunapata suluhu ya mgogoro
wa Mabwegere ambao umekuwa ukininyima usingizi,” alisema Dkt. Kebwe.
Wizara
ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ni Wizara kinara katika kutatua
migogoro ikishirikiana na wizara nyingine kwa maelekezo ya Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli.
0 maoni:
Chapisha Maoni