Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amemwelekeza Mkuu wa Jeshi la Polisi, IGP Ernest Mangu kuwahamishia Utumishi baadhi ya wafanyakazi wa jeshi hilo ambao si askari ili kujenga nidhamu ya kijeshi katika wizara hiyo.
Rais Magufuli alitoa agizo hilo Ikulu jijini Dar es Salaam, mara baada ya kushuhudia kiapo cha uadilifu kwa viongozi wa umma kwa askari 58 wa jeshi la Polisi waliopandishwa vyeo hivi karibuni.
Alilazimika kutoa agizo hilo kufuatia tukio la kusimamishwa kazi kwa Mhasibu Mkuu wa Jeshi la Polisi, Frank Charles Msaki kutokana na tuhuma za kufanya malipo hewa huku akidaiwa kutumia madaraka yake vibaya.
Wahamishieni kule Utumishi wale wakorofi ili hawa raia wanaofanya kazi kwenye nafasi za jeshi waondoke, kwani hakuna askari wanaojua masuala ya fedha? Huwezi ukachanganya askari na wafanyakazi wasio askari.Naomba IGP uliangalie vizuri hili ili raia ambao wanasumbua jeshi uwapeleke Utumishi alisema Rais Dkt. Magufuli.
Akifafanua kuhusu mhasibu aliyesimamishwa, Rais Magufuli alisema mhasibu huyo alikuwa na mamlaka hata ya kuwakemea askari, ndipo alipotoa agizo asimamishwe na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.
Kwa upande mwingine, Rais Magufuli amemuagiza IGP kufuatilia taarifa inayodai kuwa kuna mfanyabiashara aliyelipwa mabilioni na Jeshi hilo bila ya kutoa huduma ya kushona sare za askari.
Alisema taarifa za mfanyabiashara huyo zinadai kuwa alilipwa kati ya Shilingi bilioni 20 hadi 60 bila ya kutoa huduma hiyo, huku jeshi la Polisi likiwa halijatoa taarifa yoyote kuhusu madai hayo.
Alisema wakati fedha hizo zikidaiwa kulipwa bure, fedha hizo zingeweza kusaidia jeshi hilo kulipia kodi magari yake 77 yanayodaiwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Pamoja na maagizo hayo, Rais Dkt. Magufuli alieleza kuridhishwa na utendaji kazi wa jeshi hilo na kueleza kuwa kutokana na hali hiyo aliona ni wajibu wake kuwapandisha vyeo askari ambao utendaji kazi wao ni wa kuridhisha.
Hata hivyo alisema alilazimika kuyaondoa majina ya askari 17 kati ya askari 60 waliopandishwa cheo cha Kamishna Msaidizi Mwandamizi (6) na Kamishna Msaidizi wa Polisi (11) kutokana na kutoridhishwa na utendaji kazi wao.
Aliwataka makamanda hao wa Jeshi la Polisi kuhakikisha hakuna wafanyakazi hewa kwenye maeneo yao ili fedha zinazotumika kulipa wafanyakazi hao zitumike kuboresha maslahi ya askari wa jeshi hilo.
Naye Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba aliwataka askari waliopandishwa cheo kwenda kushughulikia matatizo ya wanyonge badala ya kuwashughulikia wanyonge waliopo kwenye maeneo yao ya kazi.
Alisema changamoto kubwa iliyo mbele yao ni kuhakikisha wanakomesha vitendo vya wananchi kuchukua sheria mikononi kwa kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia sheria na uadilifu na hivyo kuthibitisha uwezo wao kwa Rais aliyewapandisha cheo.
Kwa upande wake, Kamishna wa Maadili Jaji Mstaafu Salome Kaganda, alisema askari waliokula kiapo cha uadilifu wanapaswa kuthibitisha kiapo hicho kwa kutekeleza majukumu yao kwa kusimamia vizuri amana za Serikali na kuzingatia maadili ya utumishi na uzalendo.
Aliwataka makamanda wa Polisi kuhakikisha kunakuwepo kamati za maadili katika maeneo yao kuanzia ngazi za wilaya na mikoa ili kurahisisha utekelezaji wa majukumu yao kwa kuzingatia maadili na uadilifu.
Kwa upande wake, IGP Mangu alimuhakikishia Rais Dkt. Magufuli kuwa askari wa jeshi hilo wanazingatia maadili ya kazi yao na kwamba pale watakapokengeuka atawachukulia hatua mara moja.
Alisema kati ya askari 60 walipondishwa cheo, askari wawili Juma Abdul Yusuph na Modestus Lyimo wameshindwa kuhudhuria kiapo hicho kutokana na kuhudhuria mafunzo ya kuwajengea uwezo wa kazi zao nje ya nchi.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Meja Jenerali Mstaafu Projestus Rwegasira aliwataka askari waliopandishwa vyeo wahakikshe wanawasimamia askari walio chini yao ili watekeleze majukumu yao kwa mujibu wa sheria.
Akizungumzia kipato hicho, Kamanda wa Polisi mkoa wa Tanga ambaye amepandishwa cheo cha Naibu Kamishna wa Polisi, ACP Leonard Paulo aliahidi kutekeleza majukumu yake ikiwemo kusimamia askari walio chini yake kwa kuzingatia maadili.