Jumla
ya vijana 559 waishio katika mazingira magumu wamehitimu elimu ya
ufundi katika Chuo cha Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) chini ya
mradi unaosimamiwa na Shirika lisilokuwa la kiserikali la Plan
International.
Takwimu
hizo zimetolewa leo na Mkurugenzi wa Shirika hilo, Jorgen Haldorsen
wakati wa mahafali ya kwanza ya vijana hao yaliyofanyika katika Chuo cha
VETA, jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi
huyo amesema kuwa tatizo la ajira kwa vijana ni kubwa na linahitaji
jitihada za pamoja katika kulikabili hivyo, kwa Mkoa wa Dar es Salaam,
mradi huo unalenga kufikia vijana 2110 ndani ya miaka mitatu kutoka
Wilaya za Ilala na Temeke.
“Mahafali
ya leo ni mahsusi kwa ajili ya vijana wanaoishi katika mazingira
magumu, wamesoma fani mbalimbali za ufundi zikiwemo za umeme wa
majumbani, ushonaji, udereva, ufundi magari, uchomaji vyuma, mapishi na
mapambo ambapo zaidi ya ufundi stadi vijana wetu wamejengewa utamaduni
wa kujiwekea akiba kupitia vikundi vya hisa”, alisema Haldorsen.
Haldorsen
amefafanua kuwa uteuzi wa vijana wanaojiunga na mradi huu unafanywa na
Viongozi wa Serikali za Mitaa kwa kushirikiana na vijana wanaoishi
katika mazingira magumu kwa kufata vigezo ambavyo ni; vijana wenye
ulemavu, wasichana waliopata watoto katika umri mdogo,vijana yatima au
wanaolelewa na mzazi mmoja, vijana wanaofanya kazi na kuishi katika
mazingira hatarishi pamoja na vijana ambao hawakumaliza shule kutokana
na changamoto mbalimbali.
Naye
Mkurugenzi Mkuu wa Chuo cha Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA),
Leah Lukindo ameushkuru Umoja wa Ulaya pamoja na waandaaji na
watekelezaji wa mradi huu wakiwemo Wizara ya Vijana na Ajira, Mamlaka ya
Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi, Shirika la Plan International,
Shirika la Volunteer Service Oversees (VSO),CCBRT, UHIKI, CODERT pamoja
na uongozi wa Serikali za Mitaa kwa kuhakikisha mradi huu unaogusa
hitaji kubwa la kitaifa la ajira kwa vijana unafanikiwa.
Wakiwasilisha
ujumbe kwa njia ya risala,vijana waliohitimu mafunzo hayo wamesema kuwa
wamepata msaada na ushauri ambao umewajengea ujasiri wa kuweza
kujiajiri wenyewe na hata kuajiriwa kutokana na fursa zilizopo na
zitakazojitokeza.
Mradi
huu unatekelezwa katika Mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro, Pwani, Lindi
na Mtwara kwa kipindi cha miaka mitatu, mradi huo unagharimu kiasi cha
Euro 3,874,984.53 na unafadhiliwa na Umoja wa Jumuiya ya Nchi za Ulaya.
0 maoni:
Chapisha Maoni