Wizara
ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto inampongeza
Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kwa kupiga
marufuku matumizi ya Shisha na uvutaji wa Sigara hadharani kama afua ya
kupunguza madhara ya tumbaku na madawa ya kulevya katika jamii.
Uchunguzi wa kitalaam uliofanyika
umebaini kuwa Shisha ina madhara kwa afya ya watumiaji hasa vijana na
watoto. Watumiaji wa Shisha wanatumia kiwango kikubwa cha tumbaku kwa
muda mfupi, hali inayoongeza madhara yatokanayo na tumbaku kama vile: –
Saratani, Magonjwa ya Mapafu, Kibofu cha mkojo, Tezi dume, Koo, Mdomo na
Kiywa, Ngozi, Ini, Ubongo.
Pia imebainika kwamba matumizi ya
Shisha huambatana na kuongezewa dawa nyingine za kulevya na hivyo
hufanya watumiaji wa Shisha kupata uraibu wa dawa za kulevya. Matumizi
ya dawa hizo za kulevya ni kosa la jinai.
Wizara ya Afya, Maendeleo ya
Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto inapenda kurejea na kusisitiza agizo lake
la tarehe 12 Machi 2015 la kuzuia matumizi ya sigara na matumizi ya
bidhaa za tumbaku katika maeneo ya umma
Inakumbushwa kwamba agizo hili
limezingatia utekelezaji wa Sheria ya Usimamizi wa Bidhaa za Tumbaku,
Sura ya 121 T.L 2002, ya Sheria za Tanzania kipengele cha 12 (1) ambacho
kinakataza matumizi ya Tumbaku katika Maeneo ya Umma.
Madhumu ya Agizo hili ni kuilinda
Jamii kwa ujumla kutokana na madhara yatokanayo na moshi wa sigara.
Wizara inawakumbusha wananchi wanaotumia bidhaa za tumbaku kupunguza au
kuacha kabisa matumizi ya tumbaku. Aidha, agizo hili linaijumuisha jamii
yote katika kubaini madhara ya tumbaku na umuhimu wa kuzuia matumizi ya
tumbaku katika maeneo ya kazi na maeneo yote ya umma.
Agizo hili linawahusu wananchi wote nchini wanaopata huduma katika maeneo ya umma kama ilivyotafsiriwa na sheria husika.
Matumizi ya tumbaku hayaruhusiwi
katika maeneo yote ya umma. Maeneo haya yanajumuisha ofisi zote za
Serikali na tasisi zake zote, watu binafsi, vyuo, vituo vya huduma za
Afya zikiwemo Hospitali, vituo vya Afya na zahanati, vituo vya usafiri
wa Anga, Mabasi, bandari na treni, sehemu za mikutano, mapumziko,
bustani na fuko za maji,sherehe,michezo,masoko,maduka makubwa pamoja na
sehemu za kuabudu.Na kwa mtu yeyote anayeendesha shughuli katika maeneo
ya umma analazimika kutenga eneo maalum kwa ajili ya wavuta sigara.
Kwa kuwa Mhe. Waziri mwenye
dhamana na masuala ya Afya nchini ameona hatari hii ya Uvutaji wa sigara
na utumiaji wa bidhaa za tumbaku kwa afya ya Wananchi, kuanzia leo
tarehe 4/7/2016 matumizi ya Shisha nchini yamepigwa marufuku kwa wote
wanaojihusisha na matumizi hayo, na kwa wafanyabiashara wote
wanaojihusisha na upatikanaji wa Shisha nchini
Hivyo basi, kwa agizo hili katika
maeneo yote nchini ambako matumizi ya Shisha hufanyika ni marufuku
matumizi hayo kuendelea kutumika.
Aidha vyombo vya Dola na mamlaka husika vinahimizwa kusimamia kwa ukamilifu katazo hili.
0 maoni:
Chapisha Maoni