Kikao cha Tume ya Pamoja ya
Kudumu ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Rwanda kilichofanyika kuanzia
tarehe 29 – 30 Aprili, 2016,kimekamilika Mjini Gisenyi, Rwanda,ambapo
wataalam wa sekta mbalimbali wameazimia kuharakisha maeneo ya
ushirikiano baina ya nchi hizi mbili.
Kikao hicho cha 14 cha
ushirikiano kimefanyika kufuatia maagizo ya Marais wa Tanzania na Rwanda
wakati wa ziara ya Mhe. Dkt. John PombeMagufuli nchini Rwanda mwanzoni
mwa mwezi Aprili mwaka huu.
Wakati wa ziara hiyo,wakuu hao
walikubaliana kuharakisha utekelezaji wa makubaliano ya ushirikiano na
kuibua maeneo mapya yanayolenga kuinua shughuli za kiuchumi baina ya
nchi hizo mbili.
Wakati wa ufunguzi wa kikao hicho
cha wataalamu kiongozi wa ujumbe wa Tanzania Balozi Ramadhan M. Mwinyi,
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Njeya Tanzania aliwakumbusha
wajumbe wa pande zote mbili kuendesha mazungumzo na mjadala kwa
kuzingatia maagizo ya viongozi hao na vilevile kuchangamkia fursa za
ushirikiano wa shughuli za kiuchumi za wananchi wa pande zote mbili
baada ya mindombinu ya kikanda kuimarika.
Kwau pande wake, Balozi Jeanine
Kambanda, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Njeya Rwanda na mwenyeji wa
kikao hicho, alihimiza wajumbe kujiwekea malengo yanayotekelezeka na
tarehe za ukomo kwenye maeneo yote watakayokubaliana ili kusukuma
utekelezaji na kupata matokeo ya haraka.
Pamoja na mambo mengine, pande
zote mbili zimekubaliana kuimarisha ushirikiano katika sekta muhimu kama
vile miundombinu ya ushorobawakati (Central Corridor), kuharakisha
ujenzi wa reli ya kati katika kiwango cha kimataifa (Standard Gauge),
kukuza ushirikiano katika sekta ya anga hususan baina ya mashirika ya
ndege ya Rwandair na ATCL, kuimarisha ushirikiano katika sekta za
sayansi na teknolojia, afya, kilimo na ufugaji, utalii, elimu,
mawasiliano n.k.
Mkutano huo pia umekubaliana
kuanzisha Kamati yaPamoja ya Utekelezaji (Joint Implementation
Committee) kwa ajili ya kufuatilia kwa karibu maeneo yote ya ushirikiano
yaliyokubaliwa katika Kikao hicho cha 14. Kamati hiyo itakayoongozwa na
Makatibu Wakuu wa Wizara za Mambo ya Nje za nchi hizo mbili, itakutana
kila robo mwaka.
Aidha, Serikaliya Rwanda
imeonesha utayari wake wakuleta nchiniMaafisa na Watumishi waSerikali
kwalengo la kupata uzoefu na mafunzo katika vyuo vya kitaalamu nchini
kama vile Chuo cha Diplomasia (CFR), Chuo cha Taifa cha Utalii na
Wanyamapori (Mweka) na Chuo cha Usafirishaji (NIT).
Kwa upande wa Tanzania, Serikali
imedhamiria kuwakutanisha wataalamu wa mitaala ya elimu kwa lengo la
kubadilishana uzoefu na Rwanda kwenye upande wa kuandaa mitaala ya elimu
ya tehama kwenye shule za awali, msingi na sekondari.
Mkutano ujao wa kuminatano waTume
ya Pamoja yaKudumu ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Rwanda utafanyika
mwaka 2018, nchini Tanzania.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa,
30 Aprili, 2016
0 maoni:
Chapisha Maoni