.DODOMA.
Serikali imesema kuwa inaendelea
na utaratibu wa kuzitambua na kuzirasimisha bandari Bubu zote
zilizokidhi vigezo ambazo zinatumiwa na wafanyabiashara kupitisha bidhaa
mbalimbali ili ziweze kuchangia katika Pato la Taifa kulingana na
wingi wa bidhaa zinazopitishwa katika bandari hizo.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi
na Mawasiliano Mhandisi Edwin Ngonyani ametoa kauli hiyo bungeni mjini
Dodoma leo wakati akijibu maswali ya Wabunge waliotaka kujua mkakati wa
Serikali katika kudhibiti bidhaa zinazoingizwa nchini na wafanyabiashara
wasio waaminifu kupitia bandari bubu hali inayoikosesha serikali
mapato.
Mhe. Ngonyani amekiri kuwepo kwa
ongezeko la wafanyabiashara wasio waaminifu wanaotumia bandari hizo
katika maeneo mbalimbali nchini hasa ukanda wa Pwani wa Bahari ya Hindi,
Ziwa Tanganyika, Ziwa Victoria na maeneo ya mipakani ambayo yanaingia
moja kwa moja kwenye makazi ya watu akieleza kuwa wengi wa
wafanyabiashara wanakwepa kodi na kutafuta urahisi wa kupitisha mizigo
yao.
Amesema maeneo hayo yamekuwa
chanzo kikubwa cha upitishaji wa bidhaa zisizokidhi viwango, Silaha na
Biashara haramu na kubainisha kuwa baadhi ya wafanyabiashara wa ndani
wasio waaminifu wamekuwa wakishirikiana na raia wa kigeni kuagiza na
kuingiza bidhaa hizo kupitia bandari hizo kwa lengo la kukwepa kodi.
Amesisitiza kuwa Serikali ya
Awamu ya tano inalishughulikia kwa nguvu zote suala hilo kupitia
watendaji wake wakiwemo wakuu wa mikoa wa maeneo husika ambao
hushirikiana na mamlaka zinazohusika vikiwemo vyombo vya ulinzi na
usalama kudhibiti njia na maeneo yote yanayotumiwa na wafanyabiashara
hao.
” Kama Serikali tunaendelea
kufanya vikao kwa kushirikiana na wakuu wa mikoa na mamlaka zinazohusika
kuangalia namna ya kurasimisha bandari bubu zilizobaki ili tuweze
kukusanya mapato ya Serikali yaliyokuwa yakipotea kutokana na wingi wa
mizigo inayopitishwa” Amesema Mhandisi Ngonyani.
Amefafanua kuwa mwaka katika
kipindi cha mwaka 2015 na mwezi Januari, 2016, doria zilizofanyika
katika maeneo yanayotumiwa na wafanyabishara hao zilifanikisha kukamatwa
kwa wafanyabiashara 98 ambao wote walichukuliwa hatua za kisheria
ikiwem mali zao kutaifishwa pamoja na kuwafikisha mahakamani.
Kuhusu bandari bubu
zilizotambuliwa na kuzirasimishwa na Serikali katika Pwani ya Bahari ya
Hindi ni Mbweni ya jijini Dar es salaam, Mlingotini mkoani Pwani,
Kisiju na Nyamisati mkoa wa Pwani na Bandari bubu ya Kilambo mkoani
Mtwara.
Aidha, amesema Serikali
inaendelea na utaratibu wa kurasimisha bandari binafsi umefanyika katika
ziwa Victoria mkoani Mwanza na maeneo mengine ambayo serikali
inaendelea kuyafanyia kazi.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa
Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Hamad Masauni amesema kuwa Serikali
inaendelea kuvijengengea uwezo vikosi vyake vya ulinzi na usalama kwa
kuviongezea vifaa vya kisasa ili viweze kuimarisha doria nchi nzima ili
kukabiliana na vitendo vyote vya uvunjaji wa sheria.
Amesema Jeshi la Polisi
linaendelea kushirikiana na wananchi kukusanya taarifa za kiharifu ili
kuwabaini na kuwakamata wafanyabishara wote wanaojihusisha na uagizaji
na uingizaji wa bidhaa kupitia bandari bubu ambaoumekua ukiisababishia
serikali ikose mapato.
” Vyombo vyetu vya ulinzi na
usalama vinaendelea kukusanya taarifa za kiharifu kutoka kwa wananchi
ili kukabiliana na wimbi hili, pia tunaendelea kuviongezea nguvu vikosi
vyetu vya ulinzi na usalama ili viweze kutimiza majukumu yao ipasavyo”
Amesisitiza Mhe.Masauni.
0 maoni:
Chapisha Maoni