Jeshi la Polisi Nchini
linawashikilia watuhumiwa 14 kufuatia tukio la mauaji ya watu watatu
lililotokea katika msikiti wa Rahman eneo la Ibanda relini mkaoni
Mwanza, Mei 18 mwaka huu.
Akiongea na waandishi wa habari
leo jijini Dar es Salaam, Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini Kamishna
Msaidizi Advera Bulimba alisema kuwa msako wa kuwakamata watuhumiwa
wengine unaendelea katika maeneo mbalimbali nchini.
Hivyo amewaomba wananchi kutoa
ushirikiano mkubwa kwa jeshi hilo ili kufanikisha kuwakamata wale wote
wanaotuhumiwa kuhusika na tukio hilo.
“Nitoe wito kwa wananchi
kushirikiana kikamilifu na vyombo vya usalama katika kufichua wahalifu
kwa kuwa ni watu tunaoishi nao, hivyo hakuna budi kutoa taarifa zao ili
usalama na mali zetu uendelee kuimarika”, aliongeza Kamishna Msaidizi
Bulimba.
Hata hivyo, alieleza kuwa hali ya
usalama nchini iko shwari na kuwatoa hofu wananchi kwamba jeshi hilo
limejipanga kikamilifu katika kuhakikisha hali ya usalama inaendelea
kuwepo.
“Niwaombe wananchi kuondoa hofu
juu ya hali ya usalama na wasiwasi na watoe ushirikiano kwa vyombo vya
dola ili kuhakikisha kwamba wote wanaojihusisha na uhalifu wanakamatwa
haraka”, alisema Kamishna Msaidizi Bulimba.
Aliongeza kuwa uchunguzi zaidi wa
matukio ya uhalifu nchini unaendelea ikiwemo matukio ya mkoani Tanga,
Dar es Salaam na mikoa mingine ili kubaini na kuwakamata wahusika na
kufikishwa katika vyombo vya sheria.
Hivi karibuni kumeripotia matukio
mbalimbali ya uvunjifu wa amani katika mikoa mbalimbali nchini ikiwemo
mauaji ya watu watatu waliouawa wakiwa msikitini jijini Mwanza.
0 maoni:
Chapisha Maoni