|
SERIKALI
imesema inakamilisha taratibu za kuanzisha mfumo wa ulinzi wa raia na
mali zao kwa njia ya mtandao wa kamera za usalama, ikianza na Mkoa wa
Dar es Salaam kwa mwaka ujao wa fedha.
Aidha,
itakamilisha taratibu za kuanzisha ukaguzi wa lazima wa magari yote
nchini pamoja na taratibu za ufuatiliaji wa magari yaendayo mikoani kwa
njia ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama).
Sambamba
na hilo, katika kusaidia kudhibiti ajali za barabarani, Jeshi la Polisi
lina mpango wa matumizi ya mfumo wa pointi na ufungaji wa kamera za
kudumu za barabarani.
Waziri wa
Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga aliyasema hayo bungeni mjini
hapa jana wakati akiwasilisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara
yake kwa mwaka wa fedha 2016/17.
Kitwanga
alisema ufungaji wa kamera za usalama (CCTV) utaanzia katika Mkoa wa Dar
es Salaam katika mwaka ujao wa fedha na kisha kuhamia mikoa mingine
nchini. Alisema katika mwaka huo, polisi itaanza rasmi kutekeleza Mpango
wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN) katika Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni kama
sehemu ya kuboresha utendaji na kuimarisha usalama wa nchi.
“Inatarajiwa
kuwa mpango huu utatekelezwa nchi nzima baada ya kubaini changamoto
zitakazotokana na utekelezaji huo katika Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni,”
alisema Kitwanga.
Kuhusu
kukabiliana na ajali, alisema ukaguzi wa lazima wa magari yote nchini
pamoja na ufuatiliaji wa magari ya mikoani kwa Tehama, utasaidia
kupunguza ajali za barabarani pamoja na kuondoa magari chakavu ili
kuweka mazingira salama.
Pia
alisema mifumo mipya ya udhibiti wa makosa ya usalama barabarani ikiwemo
tozo za papo kwa papo kwa kutumia mashine za kielektroniki umeweza
kusaidia kupunguza ajali za barabarani. Aidha, alibainisha kuwa kuna
upungufu wa ajali za barabarani kwa asilimia 13 kati ya mwaka 2014/15 na
Julai 2015 hadi Machi mwaka huu.
Alisema
katika kipindi cha Julai, 2015 hadi Machi, 2016 jumla ya ajali za
barabarani 6,984 zilitokea katika maeneo mbalimbali na watu 2,577
walipoteza maisha na wengine 7,503 walijeruhiwa.
Alisema katika kipindi kama hicho mwaka 2014/15 zilitokea ajali 8,072 na kusababisha vifo vya watu 2,883 na majeruhi 9,370.
“Upungufu
huu wa ajali ni sawa na asilimia 13. Ajali hizi zimeendelea kuleta
madhara makubwa kwa wananchi kwani idadi ya majeruhi na vifo bado ni
kubwa,” alieleza Waziri Kitwanga.
Akizungumzia
hali ya uhalifu na makosa ya jinai, Kitwanga alisema kimsingi hali ya
usalama nchini ilikuwa ya kuridhisha, kwa mujibu wa takwimu.
Alisema
katika kipindi cha Julai, 2015 hadi Machi, 2016 jumla ya makosa makubwa
53,201 yaliripotiwa katika vituo vya Polisi kote nchini ikilinganishwa
na makosa 47,942 yaliyoripotiwa katika kipindi kama hicho mwaka 2014/15
ikiwa ni ongezeko la makosa 5,259 sawa na asilimia 11.
“Ongezeko
la makosa haya yaliyoripotiwa limetokana na kusogezwa kwa huduma za
kipolisi hadi ngazi ya Kata/Shehia na kuongezeka kwa elimu ya Usalama wa
Raia kwa wananchi ambao wameelewa umuhimu wa kutoa taarifa za uhalifu
kwa vyombo vya dola,” alisema Kitwanga.
Aidha,
alisema matukio ya uvamizi wa vituo vya polisi yamepungua kutoka manane
mwaka 2014/15 hadi kufikia matukio sita mwaka 2015/16 ambayo askari
wanne na raia mmoja waliuawa na silaha 22 na risasi 273 ziliporwa.
Alisema
Jeshi la Polisi limefanikiwa kuwakamata watuhumiwa 17 waliohusika na
uvamizi wa vituo vya Polisi na kupata silaha zote zilizoporwa katika
vituo vya Stakishari, Tanga na Ikwiriri.