Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dk Leonard Akwilapo |
SHULE zote ambazo hazijasajiliwa zimepewa miezi miwili ziwe zimesajiliwa, kabla ya serikali kuzifunga baada ya muda huo kuisha.
Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dk Leonard Akwilapo alisema hayo jana.
Kwamba
ifikapo Julai 30 mwaka huu, mmiliki wa shule itakayobainika
kutosajiliwa, ikiwemo zitakazokosa vigezo vya kusajiliwa, atapaswa
kuhamisha wanafunzi waliopo kwa gharama zake.
Alisisitiza
wahusika wasajili shule hizo kabla ya tarehe hiyo. Alisema kuwa agizo
hilo ni kutekeleza Sheria ya Elimu Sura ya 353, inayoelekeza shule zote
kusajiliwa kabla ya kusajili wanafunzi.
Akwilapo
alisema kwa kutofuata utaratibu huo wa kusajili shule, wanafunzi
wanaotoka katika shule au vituo hivyo hufanya mitihani ya taifa, ikiwemo
mtihani wa maarifa (QT) na mitihani mingine ya taifa (Kidato cha Nne na
Sita) kama watahiniwa wa kujitegemea.
Alisema
pia baadhi ya wanafunzi hao huingizwa kwa utaratibu usio rasmi, kufanya
mitihani ya Darasa la Nne na Darasa la Saba katika shule zilizosajiliwa
bila kuzingatia mazingira ya mahali waliposomea, hali inayochangia kwa
kiasi kikubwa kushindwa katika mitihani hiyo.
“Wamiliki
wote wa shule ambazo hazijasajiliwa wanatakiwa kuwasilisha maombi yao
katika Ofisi za Uthibiti Ubora wa shule Kanda, Wilaya au Idara ya
Ithibati ya shule (Usajili) Makao Makuu ya wizara kabla au ifikapo Julai
30 mwaka huu,” alisema.
Alipoulizwa
ni shule ngapi ambazo zinajiendesha bila kusajiliwa, Kaimu Mkurugenzi
wa Idara ya Ithabati ya Shule, Khadija Mcheka alisema: “Hapa nilipo
sitaweza kukupa takwimu sahihi, lakini kwa mkoa wa Dar es Salaam
tumeshafungia shule za awali na msingi zipatazo 23.” “Tatizo kubwa lipo
kwenye shule za awali na msingi ndio nyingi ambazo zinatoa huduma ya
elimu bila kusajiliwa, kwa shule za sekondari ni kidogo,” alisema.
0 maoni:
Chapisha Maoni