Jeshi la polisi mkoani Arusha linamshikilia mwanafunzi wa  Mwaka wa tatu  wa chuo cha maendeleo  ya jamii Tengeru  aliyejulikana kwa jina la  Harold Mmbando (23)  mkazi wa Arusha kwa kosa la kutoa taarifa za uchochezi dhidi ya Rais wa Zanzibar Dkt. Ali Mohamed Shein na Mkuu wa Majeshi Davis  Mwamunyange  pamoja na kusambaza ujumbe wa maneno makali juu ya viongozi hao.
Akiongelea  tukio Kamanda wa polisi mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo  alisema kuwa tukio hilo lilitokea Mei, 17 mwaka huu majira ya saa 3  asubui.
Alisema kuwa mwanafunzi huyo alitoa taarifa za uchochezi kuhusu mkuu wa majeshi  ambapo alimtaka mkuu huyo wa majeshi kupindua nchi na kusema kuwa haiwezekani viongozi wote wawe  nje ya nchi huku akuna kiongozi aliyepewa mamlaka ya kukikaimu kiti.
“Mtuhumiwa huyo aliandika maneno haya, Mwamunyange pindua nchi haiwezekani wote wawe nje halafu hakuna aliyepewa mamlaka ya kukalia kile kiti, hayo ndio maneno aliyoyasema mtumiwa huyo,“ alisema Mkumbo.
Aidha aliongeza kuwa mbali na maneno hayo pia mtuhumiwa huyo  alisambaza ujumbe  mwingine wenye maneno yasemayo,
”Dk. Shein akiuawa kama Karume sitashangaa wala kustuka naomba Mungu mauaji ya kisiasa
yaliyotokea Zanzibar yawe kwaviongozi wa kisasa hasa watawala na sio wananchi
wa kawaida” hayo ndio maneno aliyoyaandika mtuhumiwa huyo kupitia  mitandao ya kijami.
Mkumbo alisema kuwa mtuhumiwa huyo atafikishwa mahakamani pindi tu upelelezi utakapo kamilika, huku akitoa  rai kwa watu wote wanaotumia mitandao ya kijamii kutumia mitandao hiyo  ya kijamii pasipo kukiuka sheria na taratibu za kisheria .
Na Woinde Shizza, Arusha