Jumatatu, 16 Mei 2016

TAMKO KUHUSU MWENENDO WA UGONJWA WA KIPINDUPINDU NCHINI LILILOTOLEWA NA MHE. UMMY MWALIMU WAZIRI WA AFYA

logo
Kila wiki serikali kupitia Wizara yangu imekuwa ikitoa taarifa ya mwenendo wa mlipuko wa ugonjwa wa Kipindupindu nchini na hatua zinazochukuliwa kudhibiti ugonjwa huu. Hadi kufikia tarehe 15 Mei 2016, jumla ya wagonjwa 21,477 wametolewa taarifa, na kati ya hao 338 wamepoteza maisha.
Ingawa kwa ujumla wake kasi ya ugonjwa wa kipindupindu imepungua ikilinganishwa na hali ilivyokuwa mwaka jana, takwimu za wiki iliyopita kuanzia tarehe 9 hadi 15 Mei 2016 zinaonesha kuwa kasi ya ugonjwa imeongezeka kidogo ambapo idadi ya wagonjwa wapya walioripotiwa wiki hiyo ni 212 ikilinganishwa na 138 walioripotiwa wiki iliyotangulia (Mei 2 hadi 8, 2016). Aidha, idadi ya vifo vitokanavyo na kipindupindu pia imeongezeka katika wiki hiyo, ambapo viliripotiwa vifo 5 ikilinganishwa na vifo 2 vya wiki iliyotangulia. Wiki iliyoanzia tarehe 9 hadi 15 Mei 2016, jumla ya mikoa minane imeripoti ugonjwa wa kipindupindu. Mikoa hiyo ni Morogoro (78), Lindi (51), Manyara (42), Dar es salaam (16), Mara (8), Pwani (8), Kilimanjaro (6) na Kagera (3). Mikoa minne kati ya hiyo iliripoti vifo vilivyotokana na ugonjwa wa kipindupindu; Lindi (2), Morogoro (1), Mara (1) na Kagera (1).
Halmashauri zilizoongoza kwa kuwa na wagonjwa wengi katika wiki hiyo iliyopita ni Kilwa (51), Kilosa (47), Babati Vijijini (33), Mvomero (23), Kinondoni (10), Mbulu (9), Kibaha Mjini (8), Morogoro Mjini (8), Tarime Mjini (8), Same (6), Temeke (6) na Bukoba Mjini (3). Halmashauri 4 ziliripoti vifo vilivyotokana na ugonjwa huu; Kilwa (2), Mvomero (1), Tarime Mjini (1) na Bukoba Mjini (1).
Kwa bahati nzuri, ugonjwa wa Kipindupindu hadi sasa haujaripotiwa kutoka mikoa ya Njombe na Ruvuma.
Takwimu hizi zinaashiria kuwa ugonjwa wa kipindupindu bado upo katika jamii tunazoishi na unagharimu maisha ya watu ambao ni nguvu kazi ya Taifa. Hivyo wote kwa pamoja hatuna budi kuendeleza juhudi za mapambano dhidi ya ugonjwa huu na tuendelee kutekeleza na kusimamia kikamilifu maelekezo na miongozo stahili inayotolewa na Wizara yangu.
Ni jambo la kusikitisha kwamba bado tunashuhudia vifo vitokanavyo na ugonjwa wa kipindupindu nchini, ambavyo vingi hutokea katika jamii. Hivyo naomba nitoe wito maalum kwa viongozi wa Vijiji/Mitaa na Kata, hasa katika maeneo yaliyoathirika, washiriki kikamilifu kuhakikisha elimu sahihi ya huduma ya kwanza kwa mgonjwa wa kipindupindu inatolewa katika maeneo yao kwa kushirikiana na wataalam wa sekta ya afya katika ngazi hizo.
Napenda kuchukua fursa hii kuwashukuru sana viongozi wa Mikoa na Halmashauri wanaosimamia kwa ukamilifu upatikanaji wa takwimu sahihi za ugonjwa huu na kutoa wito kuwa tuendelee na juhudi hizi za kutoa takwimu zenye usahihi na kwa wakati ili kuweza kusaidia kuweka mikakati thabiti ya kutokomeza kipindupindu. Aidha, Wizara inatoa rai kwa Wakuu wa Mikoa na Wilaya kushirikiana na Viongozi wa Afya wa Mikoa na Wilaya katika kuhakikisha takwimu hizi zinatolewa kwa usahihi na kwa wakati. Ni vema tukakukumbushana kuwa ufichaji wa takwimu unachangia kwa kiasi kikubwa kwa ugonjwa huu kusambaa kwa haraka na hivyo kushindwa kudhibitiwa kwa wakati.
Wizara inasisitiza kuwa kwa wakati huu ambao mvua za masika bado hazijamalizika, uwezekano wa kuongezeka kwa ugonjwa wa kipindupindu ni mkubwa, na ni lazima tuongeze juhudi za kuzuia maambukizi mapya. Kwa hiyo mikoa ambayo haina wagonjwa ni lazima wachukue hatua za tahadhari ili kuzuia maambukizi mapya. Vile vile, mikoa ambayo ina wagonjwa ni lazima iendelee kusimamia kikamilifu hatua mbalimbali za udhibiti wa mlipuko huu.

0 maoni:

Chapisha Maoni