Jumatano, 25 Mei 2016

MACHINGA, MFUPA ULIOISHINDIKA HALMASHAURI YA JIJI MWANZA.

Ipo kauli isemayo “Mfupa Uliomshinda Fisi” ikiashiria jambo gumu mithiri ya mfupa mgumu ambao umemshinda fisi ambae ni mnyama bingwa wa kutafuna mifupa ya kila aina.
Ndivyo unaweza kusema ukiitazama picha hizi, kwani suala la kuzagaa ovyo kwa wafanyabiashara wadogo wadogo maarufu kwa jina la Machinga jijini Mwanza, ni mfano halisi wa mfupa ulioshindikana kutafunwa na halmashauri ya jiji la Mwanza.
 
Mara kadhaa juhudi mbalimbali zimekuwa zikifanyika ili kuwaweka wafanyabiashara hao katika mpangilio mzuri kwa ajili ya wao kufanya biashara katika maeneo rasmi yaliyotengwa lakini utekelezaji wake umekuwa wa kusuasua kwani mafanikio yake yakishindwa kuwa ya kudumu licha ya nguvu kubwa kutumika.
 
Kabla ya kipindi cha kampeni za Uchaguzi mkuu mwaka jana, halmashauri ya jiji la Mwanza ilifanikiwa kuwaondoa machinga katika maeneo yasiyo rasmi lakini baada ya kampeni kuanza, machinga walirejea mitaani kwa kasi ya ajabu na hakuna aliewagusa tena ambapo hivi sasa kila kona ya jiji la mwanza machinga wamezagaa ovyo.
 
Baadhi  ya Machinga jijini Mwanza wanaomba sekta hiyo kuboreshwa ili kuondokana na changamoto zinazowakabiri ikiwemo kukosa
maeneo maalumu kwa ajili ya wao kufanyia biashara hatua ambayo itasaidia
kuondokana na kadhia mbalimbali ikiwemo kukabiliana na mgambo wa jiji wanaokuwa
wakiwaondoa katika maeneo yasiyo rasmi kufanyia biashara

0 maoni:

Chapisha Maoni