Jumamosi, 21 Mei 2016

Serikali kutoa mafunzo maalum ya elimu ya fedha kwa wananchi


Wizara ya Fedha na Mipango imesema kuwa  iko tayari kutoa mafunzo maalum ya elimu ya fedha kwa wananchi wote wakiwemo wakinamama kuhusu ili kuleta uelewa mpana wa upatikanaji wa huduma za fedha na taratibu zinazohusu mikopo.
Kauli hiyo imetolewa leo mijini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Ashatu Kachwamba Kijaji wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum Mhe. Anna Lupembe aliyetaka kujua mipango ya Serikali ya kupeleka huduma za kibenki vijijini ili wanawake waweze kupata mikopo.
Aidha, alisema kuwa Wizara ya Fedha na Mipango kupitia Benki Kuu ya Tanzania (BOT) imehakikisha kuwa huduma za kibenki zinawafikia wananchi wengi ili kurahisisha shughuli zao mbalimbali za kiuchumi katika maeneo ya mjini na vijiji.
Alisema kuwa baadhi ya Benki zimeanzisha huduma za Kibenki kupitia mawakala, na huduma za kifedha kupitia simu za mikononi ambazo zimewasaidia wananchi kwenye sehemu ambako hakuna matawi ya Benki.
Dkt. Kijaji aliongeza kuwa  Wizara ya Fedha na Mipango kupitia Benki Kuu inaendelea kuweka mazingira wezeshi ili kusaidia nguvu za wananchi na sekta binafsi kuanzisha benki au taasisi za fedha.
Alitoa wito kwa wananchi kutumia fursa ya mazingira mazuri ya uwekezaji yaliyopo hapa nchini kuzishawishi Benki kuanzisha huduma za kibenki katika maeneo yao.
Dkt. Kijaji alisema kuwa Wizara ya Fedha na Mipango itaendelea kushawishi Benki nchini kupanua shughuli zao ili ziwafikie wananchi wengi hasa wale wa vijijini wakiwemo akina mama.
Aidha, Naibu Waziri huyo alisema kuwa Serikali kwa kushirikiana na BOT iko tayari kutoa mafunzo maalum ya elimu ya fedha kwa wananchi wote wakiwemo wakinamama kuhusu utumiaji wa huduma za kifedha ili kuleta uelewa mpana wa upatikanaji wa huduma za fedha na mikopo.

0 maoni:

Chapisha Maoni