Jumanne, 17 Mei 2016

Meya wa jiji Dar aipongeza Klabu ya Yanga kwa kunyakua Ubingwa.

indexNa Eliphace Marwa – Maelezo
Meya wa Jiji la Dare s Salaam Mh. Issaya Mwita ameipongeza klabu ya Yanga kwa kunyakua ubingwa huo kwa mara ya Ishirini na Sita tangu kuanzishwa kwa mashindano ya ligi kuu hapa nchini.
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari Mh. Mwita amesema ushindi wa Klabu ya Yanga umeliwezesha Jiji la Dar es Salaam kuendelea kupata sifa katika medani ya Kitaifa na Kimataifa kutokana na ushiriki wa klabu hiyo katika mashindano ya kimataifa.
“Ninaiomba klabu ya Yanga kuthamini ubingwa wao kwa kuonyesha viwango vya kimataifa ili kulifanya jiji hili kuwa chuo cha mafunzo ya mchezo wa mpira wa miguu,” alisema Mh. Mwita.
Aidha aliliomba Shirikisho la Mchezo wa MPira wa Miguu nchini (TFF) kuendelea kusimamia ligi kwa ustadi  zaidi ili kulingana na taratibu za mpira wa miguu kama zinavyoainishwa na Shirikisho la  Soka duniani (FIFA) pamoja na Shirikisho la Soka Barani Afrika (CAF).
“Naomba nitoe wito kwa wadau wote katika familia ya mpira wa miguu kushirikiana ipasavyo ili kufanya ligi yetu iwe miongoni mwa ligi bora barani afrika na Duniani kwa ujumla,” aliongeza Mh. Mwita.
Pia aliwapongeza wadhamini wote waliojitolea kusaidia ufadhili kwa vilabu vyote vilivyoshiriki ligi kuu na kuwataka waendelee kuwasaidia ili kuinua soka letu la bongo.
Aidha ameitakia klabu ya Yanga ya Jangwani maandalizi mema katika mchezo wa marudiano wa kufuzu hatua  za makundi ya kombe la Shirikisho la mpira wa miguu Barani Afrika (CAF) dhidi ya klabu ya Sagrada Esperance huko nchini Angola.

0 maoni:

Chapisha Maoni