Serikali imewahakikishia wananchi
kuwa inaendelea na utekelezaji wa mpango wa ujenzi wa zahanati kila
kijiji, vituo vya afya kila kata na Hospitali katika kila Wilaya ikiwa
ni mkakati wake wa kuboresha huduma za afya kote nchini.
Hayo yamesemwa leo bungeni mjini
Dodoma na Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za
Mitaa (TAMISEMI) Mhe. Suleiman Jafo wakati akijibu swali la Mbunge wa
Busokelo Mhe. Fredy Mwakibete kuhusu Mpango wa kujenga zahanati kila
Kijiji na kituo cha afya kila Kata.
Mhe. Jafo alisema kuwa Serikali
kwa kushirikisha nguvu za wananchi inaendelea na ujenzi wa zahanati,
vituo vya afya na Hospitali kila Wilaya ambapo ujenzi huo unafanyika
chini ya Mpango wa Maendeleo ya Afya ya Msingi (MMAM).
“Utekelezaji wa Mpango huo
unaendelea na kwenye bajeti ya mwaka wa fedha 2016/2017 Halmashauri
zimetengewa shilingi bilioni 182.5 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya
afya na kipaumbele kitatolewa katika kukamilisha miradi viporo badala
ya kuanzisha miradi mpya.” alisema Jafo.
Kwa mujibu wa Mhe. Jafo, Ofisi
ya Rais TAMISEMI inafanya tathmini ya utekelezaji wa mpango wa MMAM ili
kujua idadi ya Vijiji ambavyo havina zahanati, Kata ambazo hazina vituo
vya afya na Wilaya ambazo hazina Hospitali lengo likiwa ni kuhakikisha
maeneo hayo yanapewa kipaumbele na kutengewa fedha ili kusogeza huduma
za afya karibu na wananchi.
Akieleza mafanikio ya mpango wa
MMAM, Mhe. Jafo alisema kuwa chini ya mpango huo vituo vya kutolea
huduma za afya vimeongezeka kutoka 5,255 mwaka 2006/2007 hadi 6,935
mwaka 2014/2015 sawa na ongezeko la asilimia 39.9 hivyo kuna matumaini
makubwa ya kuvifikia vijiji vingi kupitia mpango huo.
0 maoni:
Chapisha Maoni