……………………………………………………………………………………………………
Na. Mwandishi Wetu
Ofisi ya Waziri Mkuu imejadili na
kuboresha rasimu ya Kiswahili ya Mpango wa Halmashauri wa Kujiandaa na
Kukabiliana na Maafa wilayani Kilosa Mei 30, 2016.
Rasimu hiyo imejikita katika
kutoa miongozo ya uratibu katika kukabili dharura za aina zote za
majanga yanapotokea katika ngazi zote za Kitaifa.
Akizungumza na wajumbe wa Kamati
ya Maafa Wilayani Kilosa Mkurugenzi wa Tafiti na Mipango Idara ya
Uratibu wa Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu, Bi. Naima Mrisho alieleza kuwa
muongozo huo ni sehemu ya kuisaidia jamii katika kupata mbinu bora
za kujiandaa, kukabili, na kurejesha hali pindi maafa yanapotokea ili
kuzisaidia jamii zetu.
“Ni muhimu kuwa na mpango huo kwa kuzisaidia Halmashauri zetu katika kupambana na maafa yanayotukabili,”alisema Bi. Naima
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya
Kilosa Mhe. John Henjewele alibainisha umuhimu wa Mpango huo ikiwa ni
sehemu ya kuanzia na inayotoa muongozo mzuri unaosaidia katika
Halmashauri yake katika kukabiliana na Maafa.
“Tangu mpango kuanza kutumika
Desemba 2013 Wilaya ya Kilosa imeweza kuwa na mbinu za kuyakabili maafa
yanapotokea hususani yale ya mafuriko” Alisema Mkuu wa Wilaya.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya
Wilaya ya Kilosa Bw. Idd Mshili aliipongeza Ofisi ya Waziri Mkuu kwa
kuona umuhimu wa kuitembelea Halmashauri yao kwa kuupitia Mpango na
kuuboresha ili kusaidia kurahisisha uelewa kwa kua lugha ya Kiswahili
inaeleweka kwa urahisi hususani ngazi ya chini na kwa wanavijiji
wanaokumbana na maafa pindi yanapotokea.
“Nichukue fursa hii kuwapongeza
Idara ya Uratibu wa Maafa kwa kuona umuhimu wa kuubadili mpango kutoka
lugha ya Kingereza kuwa katika lugha ya Kiswahili ili kufikia makundi
yote ya jamii kwa urahisi.”
AWALI: Mpango wa Halmashauri wa
Kujiandaa na Kukabiliana na Maafa ulianza kutumika mwaka 2013 ikiwa na
lengo la kuziwezesha Halmashauri kujiandaa na kuyakabili maafa
yanapotokea, Ofisi ya Waziri Mkuu imefanikiwa kufanya Tathimini kwa
Halmashauri za baadhi ya Mikoa kwa kuangalia ubora wa mpango tangu uanze
kutumika katika Mikoa ya Mtwara, Kilimanjaro, Morogoro, Dodoma, Singida
na Shinyanga kuanzia Mei 23 hadi 30, 2016.
0 maoni:
Chapisha Maoni