Jumanne, 31 Mei 2016

Serikali yaanza kutumia TEHAMA Kuendesha mchakato wa Ajira katika Utumishi wa Umma.

mae1Mkuu wa kitengo cha Mawasiliano Serikalini toka Ofisi ya Rais Sekretarieti ya Ajira Bi. Riziki Abraham (kushoto) akizungumza na Waandishi wa Habari Leo jijini Dar es salaam kuhusu utaratibu mpya wa kutumia teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika kutangaza nafasi za kazi,kupokea maombi,kuwaita kwenye usaili waombaji wa kazi na kuwapa  taarifa za kazi na kuwawezesha waombaji kupata ajira kwa kutumia mfumo huo (TEHAMA).Kulia ni Kaimu Naibu Katibu wa Sekretarieti hiyo anayeshughulikia TEHAMA Bi. Mtage Ugullum.
mae2Baadhi ya Waandishi wa Habari wakifuatilia mkutano wa Ofisi ya Rais  Sekretarieti ya Ajira uliofanyika leo jijini Dar es salaam Ukilenga kutoa taarifa kuhusu matumizi ya  teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika kuendesha mchakato wa ajira katika utumishi wa umma.
(Picha na Idara ya Habari Maelezo)
……………………………………………………………………………………………………..
Frank Mvungi-Maelezo.
Serikali imeanza kutumia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano ( TEHAMA) katika kutangaza nafasi za kazi,kupokea maombi,kuwaita waombaji kazi kwenye usaili na kuwawezesha kutumia teknolojia hiyo kupata ajira.
 Kauli hiyo imetolewa leo Jijini Dar es salaam na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini toka Ofisi ya Rais Sekretarieti ya Ajira Bi Riziki Abraham wakati wa mkutano na Vyombo vya Habari uliolenga kueleza mikakati ya Serikali kuboresha mfumo wa kupokea maombi ya ajira  na kuyashughulikia.
 “Sekretarieti ya Ajira inatoa rai kwa waombaji fursa za Ajira kujisajili katika mfumo wa Ajira unaopatikana kupitia anuani ya tovuti ya www.ajira.go.tz na mfumo wa” job alert system” au kupitia simu za kiganjani kwa kupiga *152*00# ili kuomba fursa za ajira zinazopatikana” Alisisitiza Riziki.
Akifafanua kuhusu faida za kutumia TEHAMA kuendesha mchakato wa ajira, Riziki amesema kuwa mfumo huo unasaidia kupunguza idadi ya siku za kuendesha mchakato wa ajira kutoka siku 90 hadi 52 kwa sasa.
Aliongeza faida nyingine kuwa ni Serikali inapanua wigo wa utoaji taarifa za uwepo wa fursa za Ajira hasa kwa waombaji wa ajira waishio vijijini.
Alisema mfumo huu unalenga kupunguza changamoto kadhaa zikiwemo malalamiko ya baadhi ya waombaji fursa za ajira kuhusu upotevu wa maombi yao ya kazi.
Hadi kufikia Mei, 2016 jumla ya waombaji wa fursa za Ajira waliokuwa wamejiandikisha kwenye mfumo wa utumaji maombi ya kazi walikuwa (97,765).
Aidha jumla ya waombaji wa fursa za Ajira 89,484 wamejiunga kwenye mfumo wa kupata taarifa za uwepo wa fursa za Ajira kupitia simu za kiganjani.

0 maoni:

Chapisha Maoni