Manchester United jana Jumatatu ilimtimua kazi kocha wake Louis Van Gaal kwa kile kinachotajwa kuwa ni matokeo ambayo hayawaridhishi viongozi na mashabiki wa klabu hiyo, lakini kabla hajarejea kwao kocha Van Gaal amezungumza na mtandao wa Manchester United na kuelezea hisia zake kuhusu klabu hiyo.
Van Gaal alisema kuwa imekuwa heshima kubwa kwake kupata nafasi ya kuongoza klabu kubwa kama Man United lakini pia anajivunia kuiwezesha kuchukua Kombe la FA na anaamini hilo litakuwa historia katika maisha yake.
“Ilikuwa heshima kubwa kupata nafasi ya kuongoza klabu kubwa kama Manchester United na nimefanikiwa kufikia moja ya malengo niliyojiwekea,
“Najivunia kuiwezesha kushinda Kombe la FA kwa mara ya 12 katika historia ya klabu na nina furaha katika kipindi ambacho nimefanya kazi nimeshinda mataji 20 lakini kushinda Kombe la FA ni hatua nzuri katika historia yangu, litakuwa moja ya taji kubwa katika maisha yangu,” Van Gaal aliuambia mtandao wa Man United.