Taasisi ya Josephat Torner
Foundation inayojishughulisha na watu walemavu wameiomba Serikali
kusaidia uingizaji wa mafuta ya ngozi kwa watu wenye albino nchini.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mkuu
wa taasisi hiyo Josephat Torner alipokuwa akiongea na waandishi wa
habari leo jijini Dar es Salaam ambapo alibainisha changamoto mbalimbali
zinazo wakabili watu wenye ualbino.
“Watu wengi wenye ualbino
wanaishi chini ya miaka 40 kutokana na kukosa mafuta ya kulinda ngozi
dhidi ya miale ya jua, mafuta hayo huwasaidia kutoathilika na magonjwa
ikiwemo kansa ya ngozi,” alisema Torner.
Torner alisema kuwa mafuta ya
ngozi kwa watu wenye ualbino yanauzwa kati ya shilingi 30,000 na 40,000
kwa chupa ambapo mtu mwenye ualbino mmoja anatumia wastani wa chupa tano
kwa mwaka.
Mkurugenzi huyo alisema kuwa
gharama ya mafuta hayo ni kubwa kwa watu wenye ualbino ambao wengi wao
wanaishi maisha ya chini na hasa wale wanaoishi vijijini ambao hawawezi
kumudu kuyapata na kununua mafuta hayo.
Aidha, aliongeza kuwa kama
Serikali itasaidia uingizwaji wa mafuta hayo na kupunguza ushuru ili
yaingie nchini kama madawa kupitia Bohari Kuu ya Dawa (MSD) tofauti na
hali ilivyo sasa ambapo yanatozwa kodi kama vipodozi, hatua hiyo
itasaidia kupunguza kwa kiasi kubwa kushuka bei mafuta hayo na kuwafikia
walengwa.
Kwa upande wake, Mratibu wa
taasisi ya Afrikan Albino Foundation kutoka Netherland nchini Tanzania
Bas Kreukniet amesema kuwa ikiwa Serikali itashiriki katika uingizaji wa
mafuta hayo kuna uwezekano wa mafuta hayo kuuzwa shilingi 4,000 kwa
chupa.
Aliongezea kuwa ikiwa bei ya
mafuta hayo itapungua itawasaidia watu wengi wenye ualbino hasa wa
kipato cha chini na wale waishio vijijini kutumia mafuta hayo na
kuwasaidia kujikinga na miale ya jua.
Hadi sasa taasisi ya Afrikan
Albino Foundation imeweza kuwasaidia watu wenye ualbino wapatao 13,000
tangu waanze kuleta mafuta hayo nchini mwaka 2004 ambapo kila mwezi
jumla ya chupa 5,200 huingizwa nchini kwa ajili ya kuwasaidia watu wenye
ualbino.
0 maoni:
Chapisha Maoni