Mkurugenzi
Mtendaji wa Kampuni ya Vision Investiments Ally Nchahaga (katikati)
akifafanua juu ya fursa zitolewazo na Kampuni yao leo Jijini Dar es
Salaam, kulia ni Afisa Mahusiano wa Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ)
Aisha Mohammed na kushoto ni Mkuu wa Kitengo cha Mauzo cha Kampuni ya
Mafuta ya Oil com Aluwy Amar.
…………………………………………………………………………………………………………………..
Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO
Kampuni ya Vision Investments
imetoa fursa kwa makampuni mengine kushiriki kutoa huduma mbalimbali
wakati wa makutano baina ya wanunuzi na wauzaji wa magari yanayoandaliwa
na Kampuni hiyo yatakayofanyika Mei 29 mwaka huu.
Hayo yamesemwa leo Jijini Dar es
Salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni hiyo Ally Nchahaga ambaye
amewaomba wauzaji na wanunuzi wa magari pamoja na makampuni mbalimbali
kushiriki katika makutano hayo ili kutimiza mahitaji yao ya magari.
“Kama ilivyo ada kila Jumapili ya
mwisho wa mwezi Kampuni yetu inawakutanisha wauzaji, wanunuzi wa magari
pamoja na makampuni tofauti kutoa huduma shirikishi zinazokwenda
sambamba na biashara hii ya magari ya watu binafsi” alisema Nchahaga.
Kwa mujibu wa Kampuni ya Vision
Investments makutano hayo yatafanyika nchini kwa mara ya sita ambapo
mwaka huu yatafanyika katika viwanja vya Coco Mihogo kuanzia sa 4
asubuhi.
Nchahaga alizitaja baadhi ya
kampuni zinazotoa huduma shirikishi zikiwemo Benki ya watu wa Zanzibar
(PBZ), Kampuni ya Mafuta ya Oil com, Kampuni ya Coca cola, pamoja na
Kampuni ya Simply Elegant ambazo zinatoa huduma za mikopo ya magari,
mafuta ya magari, vinywaji pamoja na vilainishi vya magari kwa wateja
watakaokuwepo katika makutano hayo.
Aidha, Nchahaga amesisitiza kuwa
kampuni yao sio ya maonyesho ya magari wala wao sio madalali bali ni
kampuni inayotoa fursa yenye gharama nafuu kwa wanachi kutimiza mahitaji
yao ya magari.
Ameongeza kuwa elimu kuhusu
magari na vifaa vyake itatolewa bure na mtu yeyote atakayehitaji kuuza
gari lake atachangia shilingi elfu 50 ikiwa ni mchango wa kuweka gari
lake katika viwanja hivyo pamoja na kufanyiwa matangazo katika mitandao
ya kijamii kwa mwezi mzima.
Naye Mkuu wa Kitengo cha Mauzo
cha Kampuni ya Mafuta ya Oil com Aluwy Amar amesema kuwa Kampuni yao
inatoa huduma mpya ya kulipa kwa kutumia kadi itakayomrahisishia mteja
kupatiwa huduma za mahitaji ya mafuta ya magari yao kwa hiyo,
watashiriki katika makutano hayo ili kutoa elimu kwa wateja hao kuhusu
matumizi ya kadi hizo.
“Huduma hii tumeianza kuitoa kwa
mikoa ya Dar es Salaam na Pwani, huduma za kupatiwa kadi pamoja na
kufanya miamala yote ni bure pia mwisho wa mwezi tutatoa huduma ya
punguzo la bei kulingana na matumizi ya mteja”,alisema Amar.
Kwa upande wake Afisa Mahusiano
wa Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ) Aisha Mohammed amesema kuwa
wamefurahi kupata fursa hii ya kushiriki katika makutano hayo kwakua
anaamini ni njia moja wapo kwa benki hiyo kuwapa mikopo au kuwanunulia
magari wateja wao ili kutimiza ndoto zao kwa muda muafaka.
0 maoni:
Chapisha Maoni