………………………………………………………………………………………………..
Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO.
Shirika la Umeme Tanzania Nchini
(TANESCO) limewataka wateja wake kuhakikisha wanaunganishiwa umeme na
mafundi au wakandarasi waliosajiliwa na shirika hilo ili kupunguza ajali
za moto.
Hayo yamesemwa leo Jijini Dar es
Salaam na Meneja wa Afya na Usalama kazini wa TANESCO, Mhandisi Majige
Mabulla alipokua akiongea na waandishi wa habari juu ya vyanzo vya ajali
za moto vinavyosababishwa na umeme.
Mhandisi Mabulla alisema kuwa
matukio ya moto yanayosababishwa na umeme hutokea kutokana na kuzalishwa
kwa joto kali ndani ya nyaya kunakosababishwa na umeme kuwa mkubwa
kuliko uwezo, kulegea kwa maungio ya nyaya pamoja na radi au nyaya za
umeme kuangukia juu ya paa la nyumba.
Kwa mujibu wa Mhandisi Mabulla
aliongeza kuwa ajali za moto zinazosababishwa na umeme huanza kama
unavyoanza moto wa kiberiti au viwashio vinginevyo vya moto na husambaa
haraka kwa kutegemea na aina ya vitu vilivyopo kwenye eneo husika kwa
kuwa baadhi ya vitu hushika moto haraka na kuenea kwa kasi.
“Ajali za moto zinazosababishwa
na umeme ni ngumu kutokea kama umeme utasukwa na mtaalam aliyebobea
kwenye fani hiyo, TANESCO tunatoa wito kwa wateja wetu kuhakikisha
wanafungiwa umeme na fundi au mkandarasi aliyesajiliwa na kampuni
yetu,”alisema Mabulla.
Pia Mhandisi Mabulla alisema ili
kuepukana na ajali za moto zinazotokana na hitilafu za umeme wateja
wanapaswa ;kuepuka kupitisha nyaya za umeme juu ya paa za nyumba,
kutokuunganisha umeme kutoka nyumba moja kwenda nyingine bila kupata
maelekeza kutoka TANESCO.
Aidha Mhandisi Mabula alisema
wateja pia wanapaswa kuhakikisha mfumo wa umeme unapitiwa upya kila
baada ya miaka mitano pamoja na kuwa makini katika utumiaji wa vifaa
vinavyotumia umeme kama vile pasi, hita za umeme.
Meneja
wa Afya na Usalama Mahali pa Kazi Kutoka Shirika la Umeme Tanzania
(TANESCO) Mhandisi Majige Mabula akiongea na waandishi wa habari (hawapo
pichani) ambapo aliwataka wateja wa shirika hilo kuzingatia sheria na
kanuni za matumizi ya umeme ili kuepuka ajali zinazoweza kusababishwa na
hitilafu za umeme.Kulia ni Afisa Uhusiano wa Shirika hilo Bw. Yasini
Silayo.
…………………………………………………………………………………………..
Frank Mvungi-Maelezo
Shirika la Umeme Tanzania
limewataka wateja wake kuzingatia sheria na kanuni za matumizi ya umeme
ili kuepuka ajali zinazoweza kusababishwa na hitilafu za umeme.
Kauli hiyo imetolewa leo Jijini
Dar es salaam na Meneja wa Afya na Usalama kazini Mhandisi Majige
Mabulla wakati wa mkutano na vyombo vya habari.
Majige amesema kuwa moto hauwezi
kutokea endapo mtumiaji wa umeme atahakikisha kuwa mfumo wa umeme
katika nyumba yake umesukwa na fundi ama mkandarasi aliyesajiliwa.
“Kuwa makini katika matumizi bora
ya vifaa vinavyotumia umeme kama vile pasi,hita za umeme,kuchaji
simu,kompyuta kutasaidia kupunguza au kuondoa tatizo la majanga ya moto”
alisisitiza Mabulla.
Akizungumzia hatua nyingine
zinazoweza kusaidia kuzuia majanga ya moto Mhandisi Majige ni kuepuka
kuweka vitu vinavyoweza kushika moto kirahisi karibu na nyaya ama
maungio ya nyaya za umeme ndani ya nyumba .
Majige alitoa wito kwa watumiaji
wa umeme kutoa taarifa pale wanapotaka kuongeza matumizi ya umeme kwa
kiwango kikubwa ndani ya makazi ya watu ili tathmini ya uwezo wa nyaya
kukidhi mahitaji yaliyoongezeka ifanyike.
Katika kuzuia matukio ya moto
TANESCO imekuwa ikihakisha kuwa inamfikishia mteja umeme ulio salama na
usiokuwa na madhara kwa mtumiaji kutoka kwenye nguzo mpaka kwenye mita.
Kwa kipindi kirefu sasa
kumekuwepo na matukio ya ajali za moto katika makazi ya watu ambayo
yamekuwa yakisababisha madhara ikiwemo kusababisha vifo,majeruhi na
uharibifu wa mali.
0 maoni:
Chapisha Maoni