Mkurugenzi
wa bendi ya African Stars, Asha Baraka akizungumza na waandishi wa
habari (hawapo pichani) kuhusiana na uzindua albamu yake ya 13
ijulikanayo kwa jina la (Usiyaogope Maisha) mkoani Mwanza kwenye ukumbi wa Villa Park Jumamosi Mei 28.
……………………………………………………………………………………………………
Na Mwandishi Wetu
Bendi ya muziki ya African Stars “Twanga Pepeta” itazindua albamu yake ya 13 ijulikanayo kwa jina la Usiyaogope Maisha mkoani Mwanza kwenye ukumbi wa Villa Park Jumamosi.
Akuzungumza jijini jana,
Mkurugenzi wa bendi hiyo, Asha Baraka alisema kuwa maandalizi ya
uzinduzi huo yamekwisha kamilika na wanamuziki wake wapo kwenye
maandalizi ya mwisho kwa ajili ya uzinduzi huo.
Mbali ya wimbo wa Husiyaogope
Maisha uliotungwa na Ali Choki, nyimbo nyingine zinazounda albamu hiyo
ni Ndoa (Luizer Mbutu), Uso Chini, (Choki), Michepuko (Msafiri Diouf),
Mapenzi Yanaumiza (Haji Ramadhani) na Ganda la Mua uliotungwa na Saleh
Kupaza ambaye kwa sasa hayupo kwenye bendi hiyo.
Asha alisema kuwa wamekwisha
rekodi nyimbo zote na mauzo ya CD 1000 ya kwanza, yatatumika kuchangia
ununuzi wa madawati mkoani humo. Alisema kila CD itauzwa Sh3, 000 na Sh
1,000 watatumia kununua madawati.
“Hii ni heshima kwa wapenzi wa
muziki wa Mwanza, bendi inafanya uzinduzi wa albamu hii kwa mara ya
kwanza mkoani, albamu zote 12 zilizinduliwa hapa Dar es Salaam, hii ni
mara ya kwanza katika historia ya bendi yetu,”
“Tunataka tuwe tofauti, mpango
wa kununua madawati pia utafanyika katika uzinduzi wa albamu hiyo kwa
mkoa wa Dar es Salaam katika siku itakayopangwa, tumepiga hesabu na
kujua dawati moja ni Sh50,000 (kama utatengeneza mwenyewe), “ alisema
Asha.
Alisema kuwa albamu hii ni ya
aina yake kwani wanamuziki wake wametunga nyimbo ambazo mbali ya
kuburudisha, pia zinatoa mafundisho mbalimbali.
Albamu za nyuma ya bendi hiyo
ni Kisa Cha Mpemba, Jirani, Fainali Uzeeni, Chuki Binfasi, Ukubwa Jiwe,
Mtu Pesa, Safari 2005, Password, Mtaa wa Kwanza, Mwana Dar es Salaam,
Dunia Daraja na Nyumbani ni Nyumbani.
Mwisho….
Caption:
Mkurugenzi wa bendi ya African
Stars, Asha Baraka akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani)
kuhusiana na uzindua albamu yake ya 13 ijulikanayo kwa jina la Husiyaogope Maisha mkoani Mwanza kwenye ukumbi wa Villa Park Jumamosi Mei 28.
0 maoni:
Chapisha Maoni