Wajumbe wa kamati ya Miss
Tanzania 2016/17 wameiomba Serikali iwasaidie kupata wadhamini wa
mashindano hayo kitaifa yanayotarajiwa kufanyika mwezi wa kumi mwaka
huu.
Ombi hilo limetolewa mwishoni mwa
wiki na Mwenyekiti wa kamati hiyo Hashim Lundenga wakati akiongea na
Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Anastazia
Wambura alipokutana nao mjini Dodoma.
Lundenga alisema changamoto kubwa
inayowakabili hivi sasa ni kupata ufadhili wa mashindano hayo ambayo
yanafaida kwa mabinti wanaoshiriki hii ikiwa ni pamoja na kujengewa
uwezo wa kuwa viongozi wazuri wa baadaye.
“Mwezi wa tisa warembo
wanatarajiwa kuingia kambini watakaa huko kwa muda wa mwezi mmoja ambako
watapewa mafunzo mbalimbali ikiwa ni pamoja kufundishwa jinsi ya
kujitambua na kujiendeleza kielimu”, alisema Lundenga.
Kwa upande wake Mhe. Wambura
aliwapongeza wajumbe wa kamati hiyo kwa kuandaa mashindano hayo na
kuwaahidi kushirikiana nao ili kuhakikisha mashindano yanafanyika kama
ilivyotarajiwa.
Mhe. Wambura alisema,
“Nawapongeza washiriki wa mashindano haya walioiwakilisha Tanzania
katika mashindano ya Dunia kwani wameweza kushika nafasi nzuri katika
mashindano ya makundi mbalimbali pia hawajawaangusha waandaaji wa
mashindano kwa kuwa wanaendelea kuisaidia jamii inayowazunguka.
Naye Miss Tanzania, Lilian
Kamazima alimshukuru Mhe. Naibu Waziri kwa kukubali kukutana nao na
kusema kuwa mashindano hayo yanaumuhimu mkubwa lisha ya washiriki kupewa
zawadi mbalimbali lakini pia wakiwa katika maandalizi ya mashindano
wanafundishwa jinsi ya kuwa wanawake wa kuigwa katika jamii, kuishi na
kuisaidia jamii inayowazunguka.
Mashindano ya Miss Tanzania Taifa
yanatarajiwa kufanyika mwezi wa kumi, hivi sasa mashindano ya vitongoji
(Vituo) yanaendelea katika maeneo mbalimbali nchini baada ya hapo
yatafuatiwa na mashindano ya Kanda.
0 maoni:
Chapisha Maoni