KAMATI
ya Utendaji ya Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania
(TASWA) ilikutana Dar es Salaam Mei 24, 2016 kujadili masuala
mbalimbali.
A; Tuzo za Wanamichezo Bora
Kikao kilikubaliana Tuzo za
Wanamichezo Bora zinazotolewa kila mwaka na TASWA, safari hii zifanyike
Agosti 26, mwaka huu, Dar es Salaam zikihusisha michezo mbalimbali.
TASWA imeuanda kamati maalum
kwa ajili ya kusimamia upatikanaji wa wanamichezo hao bora, kamati
ambayo inajumuisha waandishi waandamizi kutoka vyombo mbalimbali vya
habari na wataalamu kutoka vyama mbalimbali vya michezo. Sekretarieti ya
TASWA inaendelea kufanya mawasiliano na wateule wa kamati hiyo kabla ya
kuwatangaza.
Kwa kawaida kila mwaka TASWA
inatoa tuzo kwa wanamichezo bora wa kila mchezo na pia kunakuwa na
mwanamichezo bora wa jumla kwa mwaka husika.
Baadhi ya waliopata kutwaa tuzo
ya Mwanamichezo Bora Tanzania wa jumla kwa miaka kumi iliyopia na miaka
yao katika mabano ni Samson Ramadhani (2006), Martin Sulle (2007) na
Mary Naali (2008) wote wanariadha.
Mwaka 2009 tuzo ilienda kwa
mcheza netiboli Mwanaidi Hassan, ambaye pia alitwaa tuzo hiyo mwaka
2010, wakati mwaka 2011, ambapo tuzo yake ilitolewa mwaka 2012 mshindi
alikuwa mwanasoka Shomari Kapombe. Mwaka 2013/2014 ilienda kwa mwanasoka
Sheridah Boniface.
Mwaka 2015 tuzo ilifanyika
katika aina nyingine, ambapo walizawadiwa wanamichezo 10 tu waliofanya
vizuri zaidi katika miaka 10 ya urais wa Jakaya Kikwete na pia TASWA
ilitoa Tuzo ya Heshima kwa Kikwete.
B; Media Day
Kama inavyojulikana chama chetu
kimekuwa kikiandaa bonanza maalum likihusisha waandishi na wafanyakazi
wa vyombo mbalimbali vya habari hapa nchini, lakini kwa miaka miwili
bonanza hilo limekwama kufanyika kutokana na sababu mbalimbali. Kikao
kimekubaliana nguvu zaidi ielekezwe ili jambo hilo lifanyike na kuwapa
raha wadau. Taarifa zaidi kuhusu Media Day itatolewa Jumamosi wiki hii.
C: Changamoto kwa waandishi
Kikao kilijadili changamoto
mbalimbali zinazowakabili waandishi wa habari za michezo na chama kwa
ujumla, ambazo zimewekewa mikakati ya muda mfupi na mrefu na utekelezaji
wake utaanza kuonekana siku chache zijazo.
0 maoni:
Chapisha Maoni