JUMLA ya wanachama 950 wa
Uzinza Saccos Bank iliyoko Wilaya ya Sengerema Mkoa wa Mwanza
wamepatiwa mikopo yenye thamani ya zaidi ya Shilingi milioni 60 katika
kipindi cha mwaka 2015 .
Afisa mikopo wa Saccos hiyo
Venus Mayengela ameyabainisha hayo huko ofisini kwake Mjini Sengerema
wakati akizungumza na mwandishi wa habari hizi juu ya maendeleo
yaliyofikiwa na Saccos hiyo.
Alisema kati ya fedha hizo
zaidi ya shilingi milioni 40 zimerejeshwa , na kuongeza kwamba
wanachama waliokopeshwa fedha hizo wamo wakulima na wafanyabiashara
ndogo ndogo.
Hata hivyo alifahamisha kuwa
pamoja na elimu inayotolewa na uongozi wa Saccos kuwataka wanachama
kurejesha mikopo hiyo kwa wakati ,wapo baadhi ya wadaiwa sugu ambao
wamekuwa wakikwamisha maendeleo ya Saccos .
“Tumeweza kutoa mikopo yenye
thamani ya shilingi milioni 60,685,000 kwa wanachama wetu katika
kipindi cha mwaka jana , lakini bado changamoto ya urejeshaji wa mikopo
ni kikwazo cha maendeleo “alifahamisha .
Aidha alieleza kwamba bado
Saccos inadai zaidi ya shilingi milioni 26 ambazo ziko mikononi mwa
wadaiwa sugu ambao wamezitumia fedha za mikopo kinyume na walivyokusudia
.
Alisema ,kabla ya mwanachama
kupewa mkopo uongozi wa Saccos unafanya ukaguzi wa awali kwa anayeomba
mkopo ili kujiridhisha kwamba hakutakuwa na ugumu wa urejeshaji wake .
Akizungumzia hali za maisha
kwa wanachama waliokopeshwa alisema yamebadilika tofauti na walivyokuwa
kabla wajajiunga na Saccos na kunufaika huduma zake .
“Maisha ya wanachama
walionufaika na huduma za mikopo katika Saccos yetu zimebadilika na
biashara zao wengi wao zinazidi kukua kila siku kutokana na kuongeza kwa
mitaji yao pia “alieelza .
Hivyo aliwataka wanachama ambao
bado wanadaiwa na Saccos kurejesha fedha hizo ili kutoa fursa kwa
Uongozi kuweza kuwakopesha wanachama wengine .
0 maoni:
Chapisha Maoni