Jumanne, 24 Mei 2016

UPUNGUFU WA WAFANYAKAZI HOSPITALI YA WETE UNAWEZA KULETA ATHARI KWA MAMA WAJAWAZITO

indexNa Masanja Mabula –Pemba .
UPUNGUFU  wa wafanyakazi   kwenye  wodi ya wazazi katika Hospitali ya Wete unaweza kuleta athari kwa mama wajawazito na wazazi  kutokana na kitendo cha kutumia kitanda kimoja watu wawili .
Hayo yalibanika baada ya Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba Omar Khamis Othman kufanya ziara ya kushitukiza katika Hospitali , na kuelezea kusikitishwa na kitendo cha mama wazazi kuchangia kitanda kwa wakati mmoja .
Akizungumzia changamoto hiyo Dk Mbwana Shoka Salim alisema kuwa pamoja na uwepo wa jengo jengine ambalo limejengwa kwa ajili ya wazazi , lakini limeshindwa kutumika kutokana na upungufu wa wafanyakazi .
Awali Mkuu wa Mkoa alitaka ufafanuzi wa mama wazazi kuchangia kitanda kimoja wakiwa wawili , wakati jengo lina nafasi kubwa kutosheleza mahitaji ya mama wanakwenda kujifungua katika hospitali hiyo .
Dk Mbwana alisema , mama mzazi na mtoto  anatakiwa kuwa chini ya uangalizi wakati wote , na kwamba kitendo cha kuhamia jengo jengine itakuwa ni ufumbufu katika kutoa hudumia kwa daktari atakaye kuwa zamu .
“Jengo lipo lakini tatizo ni wafanyakazi , unajua mama mzazi na mtoto anatakiwa kuwa chini ya uangalizi wakati wote , hivyo kuwahamishia jengo jengine itakuwa ni usumbufu katika utojai wa huduma ”alifahamisha.
Naye daktari Bikombo Abdalla alikiri kwamba kitendo cha kuchangia kitanda kimoja wazazi wawili kunahatarisha maisha ya mama na mtoto kwani baadhi yao wamejifungua kwa njia ya upasuaji .
“Ni kweli hali hii inahatarisha maisha ya mama na mtoto kwani baadhi yao wamejifungua kwa njia ya upasuaji , tunaiomba Serikali ya Mkoa kusaidia kupatikana wataalamu wa kutosha ili tuweze kutoa huduma vyema ”alieleza.
Katika nasaha zake , Mkuu wa Mkoa mbali na kusikitishwa na kitendo cha wazazi kuchangia kitanda watu wawili , pia aliwataka  madaktari kutumia lugha nzuri wakati wanapotoa huduma kwa wateja wao .
Alisema , baadhi ya madaktari wanapohudumia wagonjwa hutumia lugha chafu jambo ambalo husababisha lawama kwa Serikali kutokana na kosa la mtu mmoja .
“Tumieni lugha nzuri wakati mnapohudumia wagonjwa , ili kupunguza lawama kutoka kwa wagonjwa pamoja na wananchi wanaoleta wagonjwa wao hospitalini hapa ”alisema Mkuu wa Mkoa .
Hivyo ameahidi kumchukulia hatua za kisheria daktari ambaye atabainika kutumia lugha mbaya na vitisho kwa wagonjwa .

0 maoni:

Chapisha Maoni