Wakala wa Barabara Tanzania
(TANROADS) wamekanusha kudaiwa fidia na wananchi wa Kijiji cha
Mazingira,Wilaya ya Handeni mkoani Tanga waliovunjiwa nyumba zao ili
kupisha ujenzi wa barabara.
Kauli hiyo imetolewa leo Jijini
Dar es Salaam na Meneja wa TANROADS Mhandisi Alfred Ndumbaro alipokuwa
akiongea na mwandishi wa habari hii juu ya malalamiko ya wananchi wa
Kijiji hicho kuhusu kutolipwa fidia zao.
”Sheria iko wazi kuwa wanaojenga
karibu na barabara wakivunjiwa hawalipwi fidia yoyote lakini wale ambao
ujenzi wa barabara uliwafuata katika maeneo yao wana haki ya kulipwa
fidia”, alisema Mhandisi Ndumbaro.
Mhandisi Ndumbaro ameongeza kuwa
zoezi la malipo ya fidia kwa wanakijiji waliokuwa na uhalali wa malipo
hayo lilishakwisha zamani kwa hiyo, wanaodai sasa ni wale ambao nyumba
zao zilivunjwa kutokana na kujenga eneo la barabara.
Aidha, Mhandisi huyo ametoa rai
kwa wananchi kufuata sheria za ardhi ili kupata uhalali wa viwanja vyao
pamoja na kuepuka usumbufu na gharama za kuvunjiwa nyumba zao.
Nyumba hizo zilivunjwa ili
kupisha ujenzi wa barabara ya lami yenye Kilomita 54 kutoka Mkata hadi
Handeni iliyojengwa na Kampuni ya Synohydro Corporation Limited ya
China.
0 maoni:
Chapisha Maoni