Wakili
wa Serikali Mwandamizi, Benno Sanga akifafanua kuhusu matumizi ya
sheria ya manunuzi ya umma na umuhimu wake leo Jijini Dodoma.
Baadhi ya Mawakili wa Serikali waliohudhuria semina hiyo wakisikiliza kwa makini mafunzo hayo yaliyofanyika leo Mjini Dodoma.
………………………………………………………………………………………………..
Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO
Serikali imezitaka taasisi zake
zote kufuata sheria ya Manunuzi ya Umma ya mwaka 2011 na taratibu zake
kwa manunuzi mbalimbali ya vifaa vya ofisi ili kuhakikisha fedha
iliyotumiwa inalingana na huduma iliyopatikana.
Hayo yamesemwa na Wakili wa
Serikali Mwandamizi, Benno Sanga kwenye Mafunzo ya Sheria ya Manunuzi
ya Umma ya mwaka 2011 kwa Mawakili wote nchini iliyofanyika mjini
Dodoma.
Mafunzo hayo yaliyoandaliwa na
Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, yamelenga kuwapa mawakili ujuzi
katika utoaji mzuri wa ushauri wa kisheria kwa Taasisi za Serikali.
Wakili Mwandamizi Sanga alisema
kuwa msingi mkubwa wa sheria hiyo ni ushindanishwaji wa wazabuni
unaoweza kuiletea Serikali thamani ya fedha.
“Kila taasisi ya serikali lazima
ifuate sheria ya manunuzi kwa manunuzi mbalimbali ya vifaa vya
ofisi,sheria hii imeweka utaratibu wa kuhakikisha fedha iliyotumiwa
inalingana na huduma inayopatikana”,alisema Sanga
Akitoa mafunzo hayo, Mkurugenzi
Msaidizi wa Mikataba (Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali) Bi.Monica
Otaru alisema mafunzo hayo yatawasaidia mawakili kufanya upekuzi wa
mikataba kwa makini na uhakika zaidi.
“Pamoja na kuwa kazi ya kupekua
mikataba ni sehemu ndogo ya kazi zetu lakini inachukua muda mwingi,
hivyo mafunzo haya yatawaandaa Mawakili wa Serikali walioko katika Ofisi
za Kanda kuweza kufanya upekuzi wa mikataba kwa umakini na uhakika
zaidi”,alisema Bi. Otaru.
Aidha, Bi. Otaru amezitaja baadhi
ya changamoto zinazosababisha kazi ya uhakiki wa mikataba kutofanyika
kwa usahihi zikiwemo za mikataba kukosa maelezo na maoni kamili ya
taasisi husika.
Alitaja changamoto nyingine kuwa
ni gharama za kusafirisha mikataba kutoka taasisi husika,ugumu wa njia
za mawasiliano pamoja na kutoshirikishwa kwa taasisi husika katika
mchakato wa manunuzi na uandaaji wa mikataba.
Naye Wakili wa Serikali Mwandamizi
Divisheni ya Mikataba, Said Kalunde ameelezea juu ya mambo muhimu ya
kuzingatia katika kufanya upekuzi wa mikataba ya ununuzi ikiwemo
ujazaji wa fomu mbalimbali zinazotumika katika uhakiki wa mikataba kwa
mujibu wa Sheria hiyo ya manunuzi.
“Ni muhimu sana kwa wakili
kujiridhisha kama taratibu za ujazaji wa fomu zimefuatwa na fomu
zimejazwa kwa usahihi,endapo wakili hatojiridhisha kwa kuhakiki fomu
hizo huenda akapatwa na matatizo makubwa ya kiutendaji”,alisema Kalunde.
Mafunzo hayo yametolewa kwa
mawakili wa serikali divisheni ya mikataba ili kuwajengea uwezo wa
kutekeleza jukumu la kuhakiki mikataba inayotokana na wazabuni.
Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa
Serikali imeundwa chini ya kifungu cha 59 cha Katiba ya Jamuhuri ya
Muungano wa Tanzania ambapo Mwanasheria Mkuu wa Serikali ni mshauri wa
masuala ya kisheria kwa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania
chini ya kifungu cha 59(3) cha Katiba ya mwaka 1977.
0 maoni:
Chapisha Maoni