Meneja
Uendeshaji kutoka Taasisi ya Wanawake ya Mbalawala Women
Organization inayojishughulisha na uzalishaji wa briketi za makaa ya
mawe wilayani Mbinga mkoani Ruvuma, Hajiri Kapinga (kulia) akielezea
mafanikio ya taasisi hiyo mara baada ya taarifa zake kuanza
kuchapishwa katika Jarida la Wizara. Kushoto ni Kaimu Mkuu wa Kitengo
cha Mawasilano Serikalini Wizara ya Nishati na Madini, Asteria Muhozya.
………………………………………………………………………………………………………………
Na Greyson Mwase, Dar es Salaam
Taasisi ya Wanawake ya Mbalawala inayojishughulisha na uzalishaji wa braketi za makaa ya mawe ijulikanayo kama Mbalawala Women Organization
yanye makazi yake katika kijiji cha Ruanda wilayani Mbinga mkoani
Ruvuma imeipongeza Wizara ya Nishati na Madini kupitia Kitengo cha
Mawasiliano Serikali kwa kutangaza shughuli zake hali iliyopelekea
wateja wa makaa ya mawe katika taasisi hiyo kuongezeka kadri siku
zinazokwenda.
Taasisi hiyo inayofanya shughuli
zake karibu na Mgodi wa Makaa ya Mawe wa Ngaka inajishughulisha na
utengenezaji wa briketi bora za makaa ya mawe kwa ajili ya kupikia
Pongezi hizo zilitolewa na
Meneja Uendeshaji wa Taasisi hiyo Hajiri Kapinga aliyekutana na Kaimu
Mkuu wa Kitengo cha Mawasilano Serikalini Wizara ya Nishati na Madini,
Asteria Muhozya jijini Dar es Salaam na kusema kuwa tangu Kitengo
cha Mawasiliano Serikalini kianze kuchapisha habari zinazohusu taasisi
hiyo kupitia Jarida lake linalochapishwa kila wiki lijulikanano kama MEM Newsbulletin wameshuhudia idadi kubwa ya wateja ikiongezeka na kuzidi uzalishaji wa taasisi hiyo.
Alisema kabla ya habari zake
kuchapishwa na Jarida la Wizara, taasisi hiyo ilikuwa ikiwauzia
briketi za makaa ya mawe wateja wake walioko katika vijiji
vinavyozunguka mgodi wao wilayani Mbinga mkoani Ruvuma.
“Mara baada ya taarifa zetu
kuanza kuchapishwa na Jarida la Wizara ya Nishati na Madini
tumeshuhudia mabadiliko makubwa kwani tumekuwa tukipokea simu kutoka
mikoa mbalimbali hususan Dar es Salaam, Mbeya, Iringa wateja
wakihitaji bidhaa, hali inayopelekea mahitaji kuwa makubwa kuliko
kiasi tunachozalisha,.” alisema Kapinga.
“Jarida limetufanya tujulikane,
hata wahisani wetu wameahidi kuongeza nguvu na misaada katika
kuwezesha mradi huu kuendelea vizuri; Jamii inasoma habari zetu na
sisi tumesoma masuala mengi kuhusu nishati na madini,” aliongeza
Kapinga aliendelea kusema kuwa
ili kukabiliana na mahitaji makubwa ya wateja taasisi hiyo imeweka
mkakati wa kununua mtambo mwingine kutoka nje ya nchi ili kuongeza
uzalishaji utakaoendana na mahitaji ya wateja.
Alisema mikakati mingine ni
pamoja na ujenzi wa ghala la kuhifadhia makaa ya mawe, ununuzi wa magari
kwa ajili ya usambazaji wa bidhaa ya briketi za makaa ya mawe katika
vituo vya uwakala vitakavyoanzishwa nchini karibu kila mkoa.
“Mara baada ya kuanzisha vituo
hivyo, wateja wetu watakuwa wanapata bidhaa kutoka kwa mawakala badala
ya kukutana na sisi moja kwa moja,” alisema Kapinga.
Alisema kuwa pia wamejipanga
kutoa elimu ya matumizi ya briketi za matumizi ya makaa ya mawe na
utafutaji wa masoko kwa kushirikiana na wadau wa utengenezaji wa
majiko sanifu yanayotumia briketi za makaa ya mawe kwa matumizi ya
majumbani.
Akielezea uanzishwaji wa taasisi
hiyo, Kapinga alisema kuwa taasisi hiyo ilianzishwa chini ya ufadhili
wa Mgodi wa Makaa ya Mawe wa Ngaka (Tancoal Energy Limited)
unaomilikiwa na kampuni ya Intra Energy ya Australia kwa asilimia 70 na
Serikali ya Tanzania kupitia Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) kwa
asilimia 30 ambao wanafurahishwa na hatua iliyofikiwa na taasisi hii
katika uzalishaji ya briketi za makaa ya mawe.
Aliongeza sambamba na uzalishaji
wa briketi za makaa ya mawe, taasisi hiyo imekuwa ikitoa mafunzo juu ya
utumiaji wa briketi ya makaa ya mawe katika vijiji na miji jirani na
mgodi wake pamoja na ushiriki katika maonesho mbalimbali ndani ya mkoa
wa Ruvuma.
“Lengo letu ni kuhakikisha
briketi za makaa ya mawe zinazoendelea kuzalishwa katika mgodi wetu
zinatumika majumbani, shuleni , vyuoni na taasisi mbalimbali na
kupunguza uharibifu wa mazingira kwa kutumia kuni” alisema Kapinga
Aliendelea kusema kuwa lengo la
uanzishwaji wa taasisi hiyo lilikuwa ni kuhamasisha matumizi ya nishati
mbadala kupitia briketi za makaa ya mawe na kuachana na matumizi ya
kuni ambayo ni chanzo cha uharibifu wa mazingira.
Naye Kaimu Mkuu wa Kitengo cha
Mawasiliano Serikalini, Asteria Muhozya alisema kuwa lengo la Jarida
la Wizara ni kutangaza shughuli za nishati na madini ikiwa ni pamoja
na taasisi zake
Muhozya aliongeza kuwa jarida la
Wizara lipo tayari kutangaza shughuli za wadau wa Madini na Nishati
ili kuhakikisha kuwa sekta hizo zinakuwa na kuwa na mchango mkubwa
katika ukuaji wa uchumi wa nchi
0 maoni:
Chapisha Maoni