…………………………………………………………………………………….
Na; Lucas Mboje, Rungwe
JUMLA ya Askari 327 wa
Jeshi la Magereza, kati yao wanaume 257 na wanawake 81 wametunukiwa
cheo cha Mkaguzi Msaidizi wa Magereza baada ya kuhitimu mafunzo ya
Uongozi daraja la Pili kozi namba 1 katika Chuo cha Magereza Kiwira,
Wilayani Rungwe Mkoa wa Mbeya.
Cheo hicho wametunukiwa
na Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya nchi, Meja Jenerali Projest
Rwegasira katika Sherehe za ufungaji wa mafunzo hayo zilizofanyika
katika Viwanja vya Chuo hicho leo Mei 20, 2016.
Akizungumza katika
sherehe hizo Meja Jenerali Rwegasira amesema Askari na Maafisa wa Jeshi
la Magereza nchini wanatakiwa kufanya kazi kwa kuzingatia Haki za
Binadamu na Utawala Bora kila wakati wanapotekeleza majukumu yao ya
kazi.
Jenerali Rwegasira
amesema Maafisa hao wahitimu wakazingatie elimu waliyopewa wakati wa
mafunzo ili wakawe mfano kipindi cha utendaji kazi wao ikiwa ni pamoja
na kuhamasisha na kuwaongoza wenzao ambao hawakupatiwa elimu kama yao.
Aidha, amewaasa
kutowatesa Wafungwa walioko magerezani bali kuwahudumia kwa kuzingatia
kanuni na taratibu za uendeshaji wa magereza kwani Wafungwa ni Binadamu
kama watu wengine ispokuwa tu wameikosea jamii.
“Tuzingatie falsafa ya
kwamba mfungwa yupo gerezani kwa ajili ya kutumikia adhabu na si kwa
kuongezewa adhani. Kwa kufanya hivyo, Serikali yetu itakuwa inazingatia
Utawala wa Sheria na hivyo kuwa Taifa linalozingatia na kuheshimu Haki
za Binadamu na Utawala Bora”. Alisisitiza Jenerali Rwegasira.
Akizungumza kabla ya
kumkaribisha mgeni rasmi Kamishna Jenerali wa Magereza nchini, John
Casmir Minja amesema kuwa changamoto nyingi ambazo kwa kiasi fulani
zimeathili utekelezaji wa majukumu ya Jeshi hilo ni pamoja na ufinyu wa
bajeti, makazi duni ya maafisa na askari, uhaba wa vitendea kazi na
uchakavu wa vyombo vya usafiri.
Kamishna Jenerali Minja
ameongeza kuwa tayari Jeshi hilo limechukua hatua mbalimbali za kufanya
maboresho kwa lengo la kufanya Jeshi la Magereza kuwa la kisasa katika
kutekeleza majukumu yake kisayansi na kwa ufanisi unaotarajiwa.
0 maoni:
Chapisha Maoni