Na Masanja Mabula –Shinyanga
WAKAAZI kijiji cha Ishololo Halmashauri ya Shinyanga
Vijijini wamemuomba Waziri wa Kilimo , Mifugo na Uvuvi , Mwigulu Nchemba
kufanya ziara ya kukagua ujenzi wa tuta la kuzuia maji ambalo limeanza
kujengwa zaidi ya miaka 20 na limeshindwa kukamilika .
Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi kijijini hapo
walisema kwamba kuna harufu ya utumiaji mbaya wa fedha za ujenzi huo na
kusema suluhisho pekee ni Waziri kufanya ziara kukagua maendeleo ya
ujenzi huo .
Walisema ujenzi wa tuta hilo ulioanzishwa kwa nguvu za
wananchi ambapo mwaka 2000 Serikali ilitoa shilingi milioni 35 ,
kufanikisha ujenzi huo ili kuimarisha kilimo cha mpunga kwa wakulima
wanaozungukwa na mto huo.
“Hapa kuna majipu yanahitaji kutumbuliwa , hivyo tunamuomba
Waziri Mwigulu Nchemba kututembelea na kukagua ujenzi wa tuta hili
ambalo limeshindwa kukamilika huku serikali ikiwa imetoa fedha nyingi
”alisema Dotto Mayige .
Alifahamisha kuwa hata Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya
hiyo alifika katika eneo hilo lakini anaonekana kushindwa kulipatia
ufumbuzi tatizo hilo .
Aidha Sayi Mhoja alifahamisha pamoja na lengo zuri la
kuanzisha ujenzi wa tuta hilo , bado limeshindwa kutumika kama
lilivyokusudiwa na hivyo kuwafanya wakulima wa mpuga kutofikia malengo
waliyojiwekea.
Alieleza , mkandarasi aliepewa kazi ya ujenzi wa tuta hilo
ameodoka na kuacha vifaa (magari) vikiwa vimetelekezwa huku wananchi
wakipeana majukumu ya kuvilinda .
Aidha mwananchi mwengine aliyezungumza na mwandishi wa
habari hizi ni Malale Juma ambaye alisema iwapo waziri atafanya ziara ya
kukagua ujenzi huo , ataweza kusaidia wakulima wa mpunga kutatuliwa kwa
kero zao .
“Kama hajaja Waziri hapa , ujenzi wa tuta hili
hautakamilika kwani waliokabidhiwa kusimamia wanaonekana kujalia maslahi
yao binafsi ”alieleza Malale.
Akizungumzia mavuno ya mpunga kwa msimu huu alisema baadhi
ya wakulima wamepata hasara baada ya mvua ya mawe kunyesha na kuharibu
mazao yao ambapo mavuno yameshuka kwa asilimia 98.
“Wapo baadhi ya wakulima ambao walikuwa wamepanga kuvuna
magunia 10 , wamevuna debe moja , baada ya mvua kubwa iliyokuwa
imeambatana na mawe kupukutisha mpunga ukiwa shambani ”alifahamisha.
Kukamilika kwa ujenzi wa tuta hilo kutawawezesha
wakulima wa Mpunga kuendesha kilimo kwa njia ya umwagiliaji na hivyo
kukabiliana na tatizo la njaa linaakabili.
0 maoni:
Chapisha Maoni