SPIKA Mstaafu wa Bunge la Jamuhuri ya
Muungano Tanzania, Anne Makinda amesema kuchaguliwa kwa Dk John Magufuli kuwa
Rais wa awamu ya tano kumewanusuru watanzania na machafuku yaliyokuwa
yakielekea kutokea kwasababu ya tofauti kubwa ya vipato baina ya masikini na
matajiri iliyokuwa ikiendelea kutokea.
Akizungumza na wanahabari kwenye mkutano
uliokuwa unapitia utekelezaji wa program ya Ukanda wa Kuendeleza Kilimo
Kusini mwa Tanzania (SAGCOT) katika kongani ya Ihemi inayohusisha mikoa ya
Iringa na Njombe, Makinda alisema:
“Tungeendelea tulivyokuwa
tunaendelea, hakika tungekuja kuuana kwasababu wenye nacho waliendelea kupata
zaidi na wasionacho waliongezeka kwa kuwa watumwa wa wenye nacho,” alisema.
Makinda alisema bahati mbaya iliyokuwa ikilikumba
Taifa, baadhi ya matajiri ambao wengine hawaeleweki wanafanya kazi gani, walifikia
mafanikio waliyonayo kutokana na ujanjaunja wa kunufaika kijanjajanja na fedha
za serikali.
“Kuna watu walikuwa hawaeleweki wanafanya kazi
gani, lakini ni mamilionea, baadhi yao ndio wale walikuwa wananufaika na
mamilioni ya serikali,” alisema.
Akipongeza staili ya Dk Magufuli ya kuiweka nchi
sawa katika Nyanja mbalimbali, Spika huyo mtaafu alisema kila mtanzania ataonja
machungu yatakayokuja kuliponyesha taifa mbele ya safari.
“Kutakuwa na magumu, wengi watasema aaha
huyo bwana mbona kabana hivi, lakini ni muhimu watanzania wakajua hii ni
oparesheni kubwa itakayotuumiza wote, lakini mwisho wa yote Taifa na watanzania
tutapona,”alisema.
Makinda aliwataka watanzania waendelee
kumuombea kwa Mungu, Dk Magufuli ili aendelee kuwa na afya njema, busara na
afanye kazi kwa kasi aliyoanza nayo hadi atakapomaliza awamu yake ya kwanza ya
miaka mitano.
Akizungumzia maisha yake binafsi baada ya
kutoka kwenye siasa, alisema anajishughulisha na kilimo na akataja mazao mawili
ya biashara anayolima kuwa ni pamoja na chai na mpunga.
Makinda ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi
ya Chai alisema anafurahia kufanya kazi ya kuwatetea wakulima wa chai nchini na
akaahidi kuhamasisha kwa nguvu zake zote uzalishaji zaidi wa zao hilo.
“Kama bodi ya chai, tunahamasisha uanzishaji wa viwanda katika maeneo yote yanayolimwa chai ili kuongeza tija katika kilimo hicho,” alisema na kutaja maeneo hayo kuwa ni pamoja na Njombe, Kilolo na Tarime.
0 maoni:
Chapisha Maoni