Benki ya Maendeleo ya Kilimo
Tanzania (TADB) imeiomba Serikali kupitishia fedha zote za maendeleo
katika sekta ya kilimo katika Benki hiyo ili ziweze kuwafikia walengwa
kwa urahisi zaidi.
Kauli hiyo imetolewa leo mjini
Dodoma na Mkurugenzi Mwendeshaji wa TADB Thomas Samkyi wakati akitoa
taarifa yake ya utangulizi kwenye semina ya wabunge wa Bunge la Jamhuri
Muungano wa Tanzania kuhusu kuanzishwa kwa TADB na majukumu yake.
Alisema kuwa hatua hiyo
itasaidia Benki hiyo kuwa imara ili iweze kutoa huduma zinazotarajiwa
kwa wakulima ambao wengi wako vijijin .
Samkyi aliongeza kuwa kuimarika
kwa Benki hiyo kutaiwezesha kutoa mikopo kwa wakulima wengi hasa wa
vijijini ambao hawawezi kupata mikopo au mitaji katika Benki za biashara
wala kuhimili gharama zake.
Alisema kuwa mtaji uliopo ni
kidogo ambao benki hiyo haiwezi kukopesha miradi mikubwa wala mikoa
mingi kwa muda mrefu kwani itakosa ukwasi katika kipindi kifupi.
Aida ,Mkurugenzi huyo alisema
kuwa pamoja na uhaba wa mtaji TADB imeweza kutoa elimu kwa wakulima
45,987 ili waweze kupatiwa mikopo.
Naye Mkurugenzi wa Mipango,
Utafiti na Sera wa TADB Francis Assenga Benki hiyo imeiomba Wizara ya
Fedha na Mipango kuweka angalau tengo la shilingi bilioni 200 katika
bajeti ya mwaka ujao wa fedha wakati taratibu za hati fungamani
zikikamilishwa.
Aliongeza kuwa Benki hiyo iliweza kuwekeza sehemu ya mtaji uliopatikana kwenye masoko ya fedha na kupata faida kidogo.
Kwa upande wa Mkurugenzi wa
Mikopo na Biashara wa TADB Robert Pascal alitaja maeneo 14 ya kipaumbele
ya bidhaa za kilimo ambazo zinaweza kupatiwa mikopo kuwa ni kilimo cha
nafaka, kilimo cha mazao ya viwanda(miwa na korosho) na ufugaji wa
ng’ombe.
Maeneo mengine ni kilimo cha
mbogamboga(matunda,mboga mboga na viungo) na kilimo cha mbegu za mafuta
,kilimo cha mazao ya misitu(ufugaji wa nyuki) , ufugaji wa kuku wa
kienyeji na kuku wa kisasa na ufugaji wa samaki.
0 maoni:
Chapisha Maoni