Jeshi  la polisi mkoani Singida linamshikilia mlinzi wa nyumba ya mkuu wa wilaya ya Manyoni,  Saidi Abdala (49) kwa tuhuma ya kuvunja nyumba ya mwajiri wake DC Cosmas Pascal na kisha kuiba mali mbalimbali ambayo kwa sasa bado haijafahamika na thamani yake haijajulikana.
Kamanda wa polisi mkoa wa Singida, ACP Thobias Sedoyeka, alisema tukio hilo limetokea juzi saa 12.00 jioni huko Manyoni mjini.
Alisema siku ya tukio DC Pascal alipigiwa simu na mlinzi wake Said, kwamba nyumba yake imevunjwa mlango wa mbele na vitu mbalimbali vimeibwa.
“Kwa sasa tunamshikilia mlinzi huyo kwa mahojiano zaidi ili kulisaidia jeshi katika kuwapata wahusika wa tukio hilo. Nitoe wito kwa raia wema kutoa ushirikiano kwa kutoa taarifa zitakazosaidia kuwakata watu waliohusika na tukio, waweze kukamatwa na sheria ichukue mkondo wake,” alisema Sedoyeka.
Katika matukio mengine, Kamanda Sedoyeka alisema kuwa watu wawili wamefariki dunia katika matukio mawili tofati likiwemo la kifo cha dereva wa fuso T.209 ASQ Bakari Alli (32) ambaye haijajulikana ni mkazi wa wapi.
Alisema ajali hiyo imetokea juzi saa 11.00 jioni wakati fuso hilo likiteremka kwenye mlima Saranda wilaya ya Manyoni na kugonga basi T.439 DFL dargon linalomilikiwa na kampuni ya Leo luxury Coach, baada ya dereva Bakari kushindwa kumudu fuso kutokana na kufeli breki.
“Bakari alifariki papo hapo na abiria mfanyabiashara mkazi wa Kibaha Richard Dominick (40) alivunjika mkono wa kulia na amelazwa katika hospitali ya wilaya ya Manyoni,” alisema Sedoyeka.
Aidha, alisema katika ajali nyingine iliyotokea juzi saa mbili usiku hiko katika mtaa wa majengo Manyoni mjini, mwendesha pikipiki MC 907 ATD aina ya fekon, Riziki Samsoni (26) amefariki dunia baada ya kugongwa na lori semi trela T.599 BDD likivuta trela T.434 aina ya scania lilokuwa likiendeshwa na Noel Emmanuel (24) mkazi wa Arusha mjini.
Alisema chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva wa lori ambaye alikuwa akijaribu kupita gari lililokuwa mbele yake bila kuchukua tahadhari kwa watumiaji wengine.
Alisema kwa sasa wanamshikilia dereva wa lori Noel na baada ya kumaliza mahojiano watamfikisha mahakamani kujibu tuhuma inayomkabili.
Na Nathaniel Limu, Singida