Dodoma.
Serikali imesimamisha utoaji wa
vibali na uuzaji wa wanyama hai kutoka katika hifadhi za Taifa kwenda
nje ya Tanzania kwa kipindi cha miaka 3 mpaka hapo itakapotangazwa tena.
Waziri wa Maliasili na Utalii
Prof. Jumanne Maghembe ametoa agizo hilo bungeni mjini Dodoma wakati
akijibu hoja na michango mbalimbali ya wabunge iliyoelekezwa kwenye
wizara hiyo wakati wa Majumuisho ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya
Wizara hiyo kwa mwaka 2016/2017 ambayo imetengewa kiasi cha shilingi
bilioni 135.7.
Prof. Maghembe ameiagiza Idara ya
Wanyamapori ipange na kuweka utaratibu mpya utakaotumika kusimamia
biashara hiyo pindi itakaporejeshwa tena baada ya kumalizika kwa muda wa
zuio la Serikali la miaka 3 ikizingatia mazingira ya uhifadhi wa
wanyama hao.
USAFIRISHAJI WA WANYAMA HAI NJE YA NCHI.
Amesema kumekuwa na taarifa za
baadhi ya watanzania wasio waaminifu ambao wamekua wakijihusisha na
vitendo vya kusafirisha wanyama hai waliokatazwa kinyume cha utaratibu
jambo ambalo limeisababishia Serikali ipoteze mapato kutokana na wanyama
hao.
Kuhusu wanyama wanaoruhusiwa
kusafirishwa kama nyani, Kenge,ndege, kobe, wadudu na tumbili amesema
kuwa wamekuwa wakisafirishwa kinyume na utaratibu na baadhi ya
wafanyabiashara wasio waaminifu kwa ajili ya kutumiwa na makampuni ya
kimataifa kwenye shughuli za utafiti wa kisayansi wa tiba na chanjo.
Amesema makampuni hayo yamekuwa
yakinufaika binafsi kwa kupata fedha nyingi pindi yanapofanikiwa kupata
chanjo au tiba husika huku maeneo waliokotoka yakipata fedha kidogo
jambo ambalo serikali ya awamu ya tano imeamua kulifanyia kazi.
0 maoni:
Chapisha Maoni