Jumanne, 31 Mei 2016

Zanzibar yaadhimisha siku ya kupinga matumizi ya tumbaku duniani

indexMwakilishi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Zanzibar Dkt. Ghirmany akitoa taarifa ya Shirika hilo kwenye mkutano wa waandishi wa habari uliofanyika Wizara ya Afya Zanzibar.
Picha Na Miza Othman – Maelezo Zanzibar.
………………………………………………………………………………………………….
Na Ramadhani Ali – Maelezo Zanzibar
Inakadiriwa zaidi ya watu milioni sita duniani kote hupoteza maisha kila mwaka kutokana na athari za matumizi ya tumbaku na wanaoathirika zaidi ni vijana wenye umri wa miaka 30 hadi 39.
Akizungumza na waandishi wa habari katika Ukumbi wa Wizara ya Afya kwenye maadhimisho ya siku ya kupinga  matumizi ya tumbaku Duniani, Meneja wa Kitengo  cha maradhi yasiyoambukiza Zanzibar ndugu Omar Mwalimu Omar amesema mbali na kusababisha vifo, matumizi ya tumbaku yamekuwa chanzo kikubwa cha maradhi.
Amesema tafiti zilizofanyika zimeonyesha kuwa matumizi ya tumbaku yanachangia kwa asilimia 71 kupata saratani ya mapafu, asilimia 42 magonjwa ya njia za hewa na asilimia kumi magonjwa ya moyo.
Ndugu Omar amesema pamoja na kuwa Zanzibar haizalishi tumbaku na haina viwanda vya sigara, bado matumizi ya bidhaa hizo ni ya kiwango cha juu.
Ameongeza kuwa kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Wizara ya Afya mwaka 2011ulionyesha asilimia 7.3 ya wazanzibari kati ya miaka 25 hadi 64 ni watumiaji wa sigara na asilimia 4.1 wanatumia tumbaku kwa njia za kunusa na kuvuwata.
Meneja wa Kitengo cha maradhi yasiyoambukiza amezitaja athari nyengine zinazotokana na matumizi ya tumbaku ni kuanguka kwa uchumi wa nchi.
“Kama nilivyotangulia kusema, rika linaloathirika zaidi ni vijana wa miaka 30 hadi 39 ni wazi kuwa nchi zinapoteza nguvu kazi ambayo ipo katika umri wa kuongeza kipato cha nchi,” alisisitiza Ndugu Omar.
Amekiri kuwa katika vita vya kupambana na matumizi ya tumbaku kumejitokeza changamoto ya viwanda vinavyotengeneza bidhaa za tumbaku kuwa na nguvu kubwa ya kifedha na matumizi ya tumbaku imekuwa moja kati ya starehe hususan katika jamii ya vijana.
Amewataka waandishi wa habari kuunga mkono juhudi zinazochukuliwa na Wizara ya Afya ya kudhibiti  matumizi ya tumbaku kwa kuitanabahisha jamii juu ya athari zinazotokana na tumbaku.
Akizungumza katika mkutano huo, Mwakilishi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) aliepo Zanzibar Dkt. Ghirmany amesema Umoja wa Mataifa umepanga kila ifikapo tarehe 31 Mei ya kila mwaka iwe ni siku ya kupinga matumizi ya bidhaa zinazotokana na tumbaku ili kuitanabahisha jamii juu ya athari inayotokana na tumbaku.
Ameishauri Serikali kuandaa kanuni ya matumizi ya tumbaku ili sheria iliyotungwa ya kudhibiti uvutaji wa sigara katika maeneo ya wazi iweze kufanya kazi.
Ujumbe wa mwaka huu katika kuadhimisha siku ya kupinga  matumizi ya tumbaku Duniani ni ‘kuwa tayari kuondosha  vivutio katika paketi za kuhifadhia sigara’.

0 maoni:

Chapisha Maoni