Serikali
imesema kuwa inaendelea na utaratibu wa kuzitambua na kuzirasimisha
bandari Bubu zote zilizokidhi vigezo ambazo zinatumiwa na
wafanyabiashara kupitisha bidhaa mbalimbali ili ziweze kuchangia katika
Pato la Taifa kulingana na wingi wa bidhaa zinazopitishwa katika
bandari hizo.
Naibu
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Edwin Ngonyani
ametoa kauli hiyo bungeni mjini Dodoma leo wakati akijibu maswali ya
Wabunge waliotaka kujua mkakati wa Serikali katika kudhibiti bidhaa
zinazoingizwa nchini na wafanyabiashara wasio waaminifu kupitia bandari
bubu hali inayoikosesha serikali mapato.
Mhe.
Ngonyani amekiri kuwepo kwa ongezeko la wafanyabiashara wasio waaminifu
wanaotumia bandari hizo katika maeneo mbalimbali nchini hasa ukanda wa
Pwani wa Bahari ya Hindi, Ziwa Tanganyika, Ziwa Victoria na maeneo ya
mipakani ambayo yanaingia moja kwa moja kwenye makazi ya watu akieleza
kuwa wengi wa wafanyabiashara wanakwepa kodi na kutafuta urahisi wa
kupitisha mizigo yao.
Amesema
maeneo hayo yamekuwa chanzo kikubwa cha upitishaji wa bidhaa
zisizokidhi viwango, Silaha na Biashara haramu na kubainisha kuwa baadhi
ya wafanyabiashara wa ndani wasio waaminifu wamekuwa wakishirikiana na
raia wa kigeni kuagiza na kuingiza bidhaa hizo kupitia bandari hizo kwa
lengo la kukwepa kodi.
Amesisitiza
kuwa Serikali ya Awamu ya tano inalishughulikia kwa nguvu zote suala
hilo kupitia watendaji wake wakiwemo wakuu wa mikoa wa maeneo husika
ambao hushirikiana na mamlaka zinazohusika vikiwemo vyombo vya ulinzi na
usalama kudhibiti njia na maeneo yote yanayotumiwa na wafanyabiashara
hao.
”
Kama Serikali tunaendelea kufanya vikao kwa kushirikiana na wakuu wa
mikoa na mamlaka zinazohusika kuangalia namna ya kurasimisha bandari
bubu zilizobaki ili tuweze kukusanya mapato ya Serikali yaliyokuwa
yakipotea kutokana na wingi wa mizigo inayopitishwa” Amesema Mhandisi
Ngonyani.
Amefafanua
kuwa mwaka katika kipindi cha mwaka 2015 na mwezi Januari, 2016, doria
zilizofanyika katika maeneo yanayotumiwa na wafanyabishara hao
zilifanikisha kukamatwa kwa wafanyabiashara 98 ambao wote walichukuliwa
hatua za kisheria ikiwem mali zao kutaifishwa pamoja na kuwafikisha
mahakamani.
Kuhusu
bandari bubu zilizotambuliwa na kuzirasimishwa na Serikali katika
Pwani ya Bahari ya Hindi ni Mbweni ya jijini Dar es salaam, Mlingotini
mkoani Pwani, Kisiju na Nyamisati mkoa wa Pwani na Bandari bubu ya
Kilambo mkoani Mtwara.
Aidha,
amesema Serikali inaendelea na utaratibu wa kurasimisha bandari binafsi
umefanyika katika ziwa Victoria mkoani Mwanza na maeneo mengine ambayo
serikali inaendelea kuyafanyia kazi.
Kwa
upande wake Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Hamad Masauni
amesema kuwa Serikali inaendelea kuvijengengea uwezo vikosi vyake vya
ulinzi na usalama kwa kuviongezea vifaa vya kisasa ili viweze kuimarisha
doria nchi nzima ili kukabiliana na vitendo vyote vya uvunjaji wa
sheria.
Amesema
Jeshi la Polisi linaendelea kushirikiana na wananchi kukusanya taarifa
za kiharifu ili kuwabaini na kuwakamata wafanyabishara wote
wanaojihusisha na uagizaji na uingizaji wa bidhaa kupitia bandari bubu
ambaoumekua ukiisababishia serikali ikose mapato.
”
Vyombo vyetu vya ulinzi na usalama vinaendelea kukusanya taarifa za
kiharifu kutoka kwa wananchi ili kukabiliana na wimbi hili, pia
tunaendelea kuviongezea nguvu vikosi vyetu vya ulinzi na usalama ili
viweze kutimiza majukumu yao ipasavyo” Amesisitiza Mhe.Masauni.
Pichani
ni moja ya boti iliyokamatwa na Jeshi la Polisi Mkoani Tanga, katika
moja ya Bandari bubu ikiwa na shehena ya mizigo ya mamilioni. (Picha ya
Maktaba.
0 maoni:
Chapisha Maoni