Mkuu wa Kikosi cha Usalama
Barabarani nchini, Kamanda Mohamed Mpinga amesema mabadiliko ya sheria
ya usalama barabarani hayaepukiki ili kupunguza vifo na majeruhi
vitokanavyo na ajali za barabarani.
Kamanda Mpinga amayesema hayo leo
jijini Dar es Salaam wakati wa Uzinduzi wa Programu ya Usalama
Barabarani inayoratibiwa na Chama cha Wanasheria Wanawake Tanzania
(TAWLA) kwa kushirikiana na wadau mbali mbali wa Usalama Barabarani.
“Sheria zinazohusu masuala ya
Usalama barabarani inabidi zifanyiwe marekebisho ili ziweze kusaidia
kupunguza vifo na majeruhi kwani zilivyo sasa hazitoi adhabu kali kwa
wanaokiuka sheria hizo”alisema Kamanda Mpinga.
Aidha Kamanda huyo alisisitiza kuwa suala la Usalama Barabarani ni la kila mmoja hivyo inabidi litiwe mkazo na watu wote.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa
TAWLA, Bi Tike Mwambipile amesema chama hicho kwa kuzingatia umuhimu wa
kushughulikia masuala ya Usalama Barabarani kimeona ni vyema kikafanya
kikao hicho ili kupata mawazo ya wadau.
Bi Mwambipile amesema vifo vingi
vinavyotokana na ajali za barabarani vinawaacha wanawake wengi wakiwa
wajane na watoto yatima wanaongezeka.
Ameongeza kuwa fedha nyingi zinatumika kuwahudumia majeruhi badala ya kufanya shughuli nyingine za maendeleo ya jamii.
Naye Mwenyekiti wa TAWLA, Bi
Aisha Bade amesema mabadiliko makubwa ya sera na sheria za usalama
barabarani ni lazima yafanyike ili kupunguza athari zitokanazo na ajali
za barabarani.
Bi Bade amesema TAWLA kwa
kushirikiana na wadau wengine inafanya juhudi za makusudi ili
kuhakikisha sheria hizi zinabadilishwa ili kukabiliana na janga hili.
Visababishi vya ajali kwa hapa
nchini vimetajwa na Mratibu wa Mradi Bloomberg wa Usalama Barabarani, Bi
Mary Kessy kuwa ni ulevi, kutofunga mkanda, kutoweka vizuizi vya watoto
kwenye magari, mwendo kasi na kutovaa kofia ngumu kwa waendesha
pikipiki.
0 maoni:
Chapisha Maoni