Serikali
ya Nigeria imetangaza mpango wa kutoa ajira kwa vijana zaidi ya nusu
milioni ambao wamemaliza chuo kikuu lakini hawana ajira, hatua hii ni
mojawapo ya jitihada za serikali za kupambana na tatizo la ukosefu wa
ajira kwa vijana.
Mpango
huo ni sehemu ya uwekezaji katika jamii ulioahidiwa na rais Muhammadu
Buhari wakati wa kampeni yake ya kugombea urais. Taarifa ya Naziru
Mikailu kutoka Abuja inasimuliwa na Halima Nyanza.Mpango huo unaoitwa
N-Power Teach ni wa kwanza wa aina yake katika taifa kubwa barani
Afrika.
Ni mmoja
kati ya mikakati mitatu ambayo serikali imesema itatoa ajira za moja kwa
moja kwa watu laki tano. Watafanya kazi ya ualimu katika shule za
msingi na sekondari nchi nzima.Wale
ambao maombi yao ya kazi yatapita, wataajiriwa kwa muda wa miaka miwili
na kulipwa kiasi cha dola mia moja na kumi na tano kwa mwezi.Vile vile
watapewa komputa na vifaa vyake kamili ili ziwasaidie katika kutekeleza
majukumu yao.
Mikakati mengine miwili ni N-Power Knowledge ambao utatoa mafunzo kwa
wanigeria elfu ishirini na tano katika masuala ya teknolojia, na N-Power
Build, ambao unatarajiwa kutoa mafunzo kwa wananchi wengine wapatao
elfu sabini na tano katika maeneo ya huduma za ujenzi, mapishi, pamoja
na ufundi wa magari na masuala ya gesi.
Serikali imesema imetoa fedha za kutosha kwa ajili ya utekelezaji wa mipango hiyo katika bajeti yake ya mwaka huu.
Hata hivyo, serikali zilizopita zilikuwa na mipango mikubwa ambayo haikufaulu utekelezaji wake.
Hivyo, wengi wanataka kuona jinsi gani rais Buhari atafanikiwa katika
utekelezaji wake wakati ambapo mapato ya nchi yamepungua kutokana na
kushuka kwa bei ya mafuta duniani.
Licha ya kuwa na rasilimali nyingi, nchi nyingi za Afrika zinaishi
katika hali duni kutokana na vitendo vya ufisadi na matumizi mabaya ya
rasilimali.
|
0 maoni:
Chapisha Maoni