Mbunge wa Mbeya Mjini (Chadema), Joseph
Mbilinyi amesimamishwa kutohudhuria vikao 10 vya Bunge la 11 baada ya
kupatikana na hatia kwa kosa la kuwaonyesha wabunge kidole cha kati wakati
akitoka katika ukumbi wa Bunge.
Akisoma taarifa ya Kamati ya Haki,
Maadili na Madaraka ya Bunge iliyosikiliza na kuchunguza kesi hiyo, Mwenyekiti
wa kamati hiyo, George Mkuchika amesema wamemkuta mbunge huyo na hatia baada ya
kumuhoji na kuangalia picha za video pamoja na ushahidi uliotolewa na baadhi ya
wabunge walioona tukio hilo.
Bunge limeridhia Mbilinyi kupewa adhabu
hiyo iliyopendekezwa na kamati.
Aidha, Naibu Spika, Dkt Tulia Ackson
amewasimamisha wabunge wawili; Mbunge wa Ubungo, Saed Kubenea na Mbunge wa
Simanjiro, James Ole Millya, wote kutoka CHADEMA kuhudhuria vikao vitano vya
bunge kuanzia kikao cha leo kutokana na kusema uongo bungeni.
Kubenea amesimamishwa baada ya kubainika
kusema uongo kwamba waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt Hussein
Mwinyi kuwa ameingia Mkataba na kampuni ya China Henan International
Cooperation Group Company wa ujenzi wa nyumba za JWTZ na nyumba ya Waziri huyo
jambo ambalo sio kweli.
Naye Ole Millya amesimamishwa baada ya
kushindwa kuthibitisha ‘ushemeji’ uliopo baina ya Waziri wa Nchi Ofisi ya
Waziri Mkuu , Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu, Jenista Mhagama na
mmoja wa viongozi wa Sky Associate, inayomiliki mgodi wa Tanzanite One, Asia
Gonga aliyeolewa na Yusuph Mhagama ambaye kwa mujibu wa Millya ni ndugu wa
waziri huyo.
0 maoni:
Chapisha Maoni