Jonas
Kamaleki, MAELEZO
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa
Dkt. John Pombe Magufuli amelitaka jeshi la polisi nchini kuwadhibiti majambazi
ipasavyo kwa kuwanyanganya silaha kwenye matukio ya kiuharifu ili kukomesha
vitendo viovu katika Taifa.
Rais Magufuli ameyasema hayo leo jijini Dar es
Salaam wakati wa uzinduzi wa Mpango wa Usalama wa Jamii.
“Inashangaza jambazi anavamia kituo cha polisi anaua
na anaondoka wakati polisi wapo na wana silaha na risasi wanazo lakini
wanashindwa kumnyang’anya silaha,”alishangaa Rais Magufuli.
Ameongeza kuwa ujambazi na vitendo vya uharifu
nchini inabidi vikomeshwe mara moja ili watanzania waishi kwa amani na kufanya
maendeleo kwani wananchi wanataka maendeleo.
Akiongelea kuhusu maslahi na vitendea kazi kwa jeshi
la polisi, Rais Magufuli amesema kuwa serikali yake itafanya kila iwezalo
kuliwezesha jeshi hilo ili liweze kufanya kazi kwa ubora zaidi.
Rais Magufuli ameonyesha kuwa na imani na jeshi la
polisi licha ya kuwa na kasoro ndogo ndogo kwa baadhi ya polisi ambao wanalichafua
jeshi hilo.
Aidha ametoa agizo kwa TCRA kushirikiana na jeshi la
polisi nchini ili kuweza kurekodi simu na kutoa print out mara moja tofauti na ilivyo sasa.
Kuhusu kundi la wafanyakazi wanaofanyakazi kwenye
Dawati la Taarifa la polisi, Mhe. Rais amemtaka Mkuu wa Jeshi hilo, IGP Ernest
Mangu kuwafikiria na kuwapatia posho ya kazi kwani kazi wanayoifanya ni ngumu mno
na inahitaji umakini zaidi.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul
Makonda amemwomba Mhe. Rais kuliongezea fedha jeshi hilo ili liweze kufanya
kazi kwa ustadi zaidi na kukomesha vitendo vya uharifu nchini.
Makonda amelipongeza jeshi la polisi kwa kudhibiti
matukio ya ujambazi hapa nchini hususan kwenye mabenki.
Mpango huu wa Usalama wa Jamii umezinduliwa leo na
utadumu hadi 2019 na unatarajiwa kutoa matokeo makubwa ya kudhibiti uharifu
nchini.
0 maoni:
Chapisha Maoni