Mgahawa huu waleta mapishi mapya ya makange ya pweza, kamba (prawns) na ngisi.
Samaki
aina ya pweza amekuwa maarufu sana hapa nchini Tanzania, kutokana na
ladha yake tamu na faida zake kiafya. Kutokana na umaarufu huo vijana wa
kitanzania wameamua kuwa wabunifu zaidi na kuanzisha mgahawa wa kisasa
maalum kwa ajili ya mapishi ya pweza, kamba (prawns) na ngisi unaoitwa Pweza Cafe.
Akiongea
na mwanidishi wetu, mmoja wa wamiliki wa mgahawa huo bwana Alfred
Kiwuyo alisema, “Sisi wenyewe ni wapenzi wa supu na nyama ya pweza,
kamba (prawns) na ngisi lakini mazingira ya awali ya kuuza vyakula hivi
kwenye vituo vya daladala na makutano ya barabara kadhaa hapa jijini
yalikuwa yanatukatisha tamaa hasa ukizingatia usafi na mapishi yenyewe
haukuwa wa kuridhisha sana. Sasa tukajiuliza swali je, haiwezekani kuwa
na sehemu ya kisasa zaidi ya kuuza pweza, ngisi na kamba (prawns) na
kukawa na mapishi zaidi ya haya. Ndipo tukaamua kuanzisha mgahawa huu
ambapo tunapika mpaka makange ya pweza, prawns (kamba) na ngisi.”
Muonekano wa Pweza Cafe kwa nje.
Vivyo
hivyo akiongea na mwandishi wetu mmoja wa wateja waliofika kwenye
mgahawa huo wa kipekee nchini alisema, “Mimi nimekula makange ya pweza
na ni mara yangu ya kwanza na nimeyapenda kwa kweli, ni matamu. Kwa mara
ya kwanza nilivyosikia makange ya pweza nilishtuka kwanza nikasema
lazima niyaonje kwa kuwa tumezoea kula makange ya kuku,ng’ombe, na mbuzi
lakini sijawahi kuonja makange ya pweza.”
Watafiti
wa masuala ya kiafya wanasema, gramu 100 za nyama ya pweza ina madini
na vitamini za kutosha kwa mahitaji ya mwili wa binadamu kwa siku. Kwa
mfano kiwango hiki cha nyama ya pweza kinampatia mwanadamu mahitaji yake
ya siku ya madini ya chuma, seleniamu na vitamini B-12. Madini haya na
Vitamini hizi ni muhimu katika kuusaidia mwili kupambana na
magonjwa,kutengeneza seli hai nyekundu za damu na kuhakikisha ubongo
unafanya kazi yake vizuri.
Makange ya Prawns yakiwa tayari kwa ajili ya mteja Pweza Cafe.
Kuanzishwa kwa Pweza Cafe
iliyopo nyuma ya jengo la tume ya taifa ya Sayansi na teknolojia,
Kijitonyama ni mfano wa kuigwa kwa vijana wabunifu na wenye ndoto za
kuwa wajasiriamali nchini hivyo basi ni muhimu kwa vijana wengine
kuangalia ni biashara zipi zinaweza kuboreshwa katika jamii yetu na
kutengeneza ajira kwa vijana wengine zaidi.
Unaweza kufuatilia zaidi kuhusu mgahawa huu kwa kutembelea tovuti yao: https://www.instagram.com/pwezacafe/
Rosti ya prawns inayopatikana Pweza Cafe.
0 maoni:
Chapisha Maoni